TAARIFA VIWANDA NA UWEKEZAJI
Mkoa wa Mbeya una jumla ya viwanda 1,791 kati ya hivyo vikubwa ni 10 ambavyo ni Mbeya cement, PEPSI, Mbeya Breweries Co. Ltd, Cocacola Kwanza, Marmo E. Granito Mines (T) Ltd, Wakulima Tea Company, Katumba Tea Company, City Coffee, Tol Gases na Kapunga Rice Mills. Aidha, Mkoa una viwanda vidogo 1,734 na viwanda vya kati ni 20.
Mkoa pamoja na kutekeleza mikakati yake ya kuendeleza sekta ya viwanda kwa kuongeza ubora wa bidhaa zinazozalishwa, kuongeza uzalishaji na kutenga maeneo maalum ya viwanda. Mkoa kwa kushirikiana na wadau wengine unatekeleza mikakati ifuatayo :-
Kuongeza idadi ya viwanda vidogo kwa kuwapatia mafunzo wajasiriamali na kuwawezesha kusajili bidhaa na kupata nembo ya utambuzi wa bidhaa (barcodes). Utekelezaji wa Mkakati huu unaendelea vizuri, ambapo Halmashauri zote saba zimeingia Mkataba wa Makubaliano (MoU) na Taasisi ya GS1 Tanzania kutoa mafunzo na kuwezesha utambuzi wa bidhaa zinazozalishwa. Hadi sasa, mafunzo yametolewa kwa wajasiriamali wapatao 898 katika Halmashauri ya Chunya, Rungwe, Busokeleo, Mbeya Jiji na Kyela.
Kuendelea kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani kwa utaratibu wa Kongani (Clusters). Mkoa umeainisha minyororo ya thamani (value chains) ya viwanda ambayo ni Alizeti, Mahindi, Viazi mviringo, Ndizi, Maparachichi, Mpunga, Michichikichi, Kakao, Kahawa, Pareto, Korosho, Maziwa, Asali na Ngozi. Hadi sasa zimeanzishwa kongani ya alizeti yenye viwanda 42, Kongani ya Mpunga yenye viwanda 53, Kongani ya chakula cha mifugo yenye viwanda 3 katika Wilaya ya Mbeya.
Aidha, katika Wilaya ya Mbarali, kumeanzishwa Kongani ya Mpunga maeneo ya Igurusi na Ubaruku yenye viwanda 17 na Kongani ya alizeti Chunya yenye viwanda 19. Wilaya ya Kyela imeanzisha Kongani mbili za mpunga zenye viwanda 20 na kongani ya Mawese yenye Viwanda 5 na kongani moja yenye viwanda 4 vya sabuni. Hivyo, Mkoa umeanzisha jumla ya Kongani za aina 5 zenye jumla ya viwanda 160 vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na dihaa za mazao ya Mifugo.
Kuongeza tija kwenye Viwanda vilivyobinafsisha
Mkoa unaendelea kutekeleza agizo lako la kutathmini hali ya viwanda vilivyobinafsishwa kwa lengo la kuhakikisha kuwa viwanda hivyo vinafufuliwa au kuzalisha kwa tija ili kuongeza Uchumi wa Mkoa na Taifa na kuongeza uzalishaji wa Ajira.
Tathmini imefanyika katika viwanda 12 kama vifuatavyo: Kiwanda cha Zana za Kilimo (ZZK), Kiwanda cha Nguo Mbeya (New Mbeya Textile Mill), Kiwanda cha Nyama cha (Tanganyika Packers), Katumba Tea Company, Mwakaleli Tea Factory, Mbeya Ceramic Company, Mbeya Rice Mill & Godown, Mbeya Cement Co. Ltd, Kyela Rice Mills Ltd, Kapunga Rice Mills, Mbarali Rice Plant na Madibira Rice Mill.
Kati ya viwanda 12, viwanda 7 vinafanya kazi vizuri; Kiwanda cha nyama (Tanganyika Packers) kinatafutiwa mwekezaji; Mwekezaji wa Kiwanda cha Nguo ameamua kubadili aina ya uwekezaji baada ya kupata kibali cha Msajili wa Hazina kuwa Kiwanda cha kuzalisha mafuta ya kupikia, kutengeneza bidhaa za Wanga (starch) na chakula cha mifugo. Viwanda vya Kyela Rice Mills Ltd na Madibira Rice Mill vinahitaji wawekezaji ili kuvifufua.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki MilikiĀ©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa