Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Amos Makalla ametoa siku tatu kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela na Kampuni ya IRA General Enterprises Co. Limited kufanya mazungumzo na kumaliza mgogoro baina ya pande hizo mbili ili kukamilisha mradi wa maji wa Kapapa-Butusyo uliotelekezwa kutokana na kutokuwepo na mahusiano mazuri baini ya pande hizo mbili.
Mheshimiwa Makalla ametoa agizo alipokuwa anasikiliza kero za wananchi kupitia mikutano wa hadhara Kata ya Ipinda Wilayani Kyela baada ya wananchi kulalamikia tatizo la maji lililopo katika eneo hilo.
Makalla pia aliishauri Halmashauri kutosimamia uamuzi wa kumtaka mkandarasi kuachia mradi huo akisema kuvunja mkataba kunaweza kuisababishia Serikali hasara kubwa huku wananchi wakiendelea kuteseka kwa kukosa huduma ya maji waliyoisubiri kwa miaka mingi.
Awali Mhandisi wa maji wa Halmashauri ya wilaya ya Kyela, Amos Mtweve alisema mkandarasi huyo aliongezewa muda mara tano lakini hakukamilisha mradi huo na ndipo Halmashauri ikachukua uamuzi wa kusitisha mkataba.
Mhandisi Mtweve alisema pia uamuzi wa kusitisha mkataba ulifikiwa baada ya mkandarasi kuandikiwa barua mara kadha akiitwa lakini hakuitikia wito wala kujibu barua azizopelekewa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya IRA General Enterprises Co. Limited, Isack Usaka alikiri mradi huo kuchelewa lakini akautupia lawama upande wa Halmashauri akisema yapo mambo aliyoomba yafanyiwe marekebisho lakini hayakufanyika.
Mradi wa maji wa Kapapa-Butusyo unaotarajia kuondoa adha ya maji katika vijiji nane vilivyopo wilayani Kyela ukitokea Halmashauri ya Busokelo wilayani Rungwe,ulianza kujengwa na kampuni ya IRA Julai 2014 na ulikuwa ukamilike Januari 2015 lakini hadi sasa haujakamilika.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki MilikiĀ©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa