RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuliameutaka uongozi wa Chuo cha Sayansi na Teknolojia Mbeya kutumia wakandarasi ndani wanaosoma katika chuo hicho katika ujenzi wa majengo ya mabweni na maktaba ili yakamilike kwa wakati.
Mhe. Rais Magufuli ameyasema leo katika sherehe za uwekaji jiwe la msingi ujenzi wa maktaba na kuwapongeza Viongozi wa MUST kwa lengo la kupanua udahili wa wanafunzi kutoka 4630 wa sasa hadi kufikia 15000 ifikapo 2025.
Mhe.Rais Magufuli ameahidi kutoa shilingi bilioni 2.9 na kuwataka viongozi wa chuo kutumia wakandarasi ambao wamekuwa wakitumika kujenga majengo mbalimbali ya Serikali ikiwemo shule kongwe 15, vyuo vya maendeleo ya wananchi 18, hospitali na majengo ya wizara Mkoani Dodoma.
Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali itahakikisha chuo hicho kinaimarishwa ili kutimiza ndoto ya Baba wa Taifa Hayati Mwl Julius Kambarage Nyerere aliyetaka Taifa liwe na chuo imara cha Sayansi na Teknolojia na kutokana na dhamira hiyo Serikali itatoa shilingi 5 bilioni kwaajili ya Ujenzi wa mabweni ya wanafunzi, na kuiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kutafuta fedha za kununulia vifaa vya kufundishia na kujifunzia wanafunzi.
Aidha, Mhe Rais Magufuli amekipongeza chuo cha MUST kwa kuanzisha mafunzo ya ufundi mchundo na usadifu na kuwaonya wanafunzi wa chuo hicho kuelekeza jitihada zao katika masomo badala ya masuala yasiyo ya msingi ikiwemo mahusiano ya kimapenzi
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe Prof. Joyce Ndalichako amemshukuru Mhe Rais Magufuli kwa kutoa kipaumbele katika elimu na amebainisha kuwa pamoja na kujengwa maktaba hiyo Serikali imetoa sh. Milioni 482.6 kwa ajili ya Ujenzi wa vyumba vya madarasa vya chuo hicho, imetoa sh milioni 702 kwa ajili ya kukarabati majengo ya chuo cha MUST kampasi ya Rukwa na sh. Milioni 483 kwa ajili ya kujenga mabweni ya wanafunzi 600 katika kampasi ya Rukwa.
Prof. Ndalichako ameongeza kuwa katika jitihada za kuboresha miundombinu ya vyuo vya elimu ya Juu Serikali imetoa shilingi bilioni 10.2 kwa ajili ya kujenga mabweni ya Chuo Kikuu cha Mzumbe Mkoani Morogoro, ametoa shilingi bilioni 3 kwa ajili ya kujenga jengo la Taaluma na Utawala na shilingi milioni 488.3 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya kampasi ya Tegeta Dar-es-Salaam. Akisoma taarifa ya Chuo hicho Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Aloys Mvuma maktaba hiyo ina ghorofa 3 na uwezo wa kuchukua wasomaji 2500 kwa mara moja ikilinganishwa maktaba iliyopo hivi sasa ambayo inachukua wasomaji 150
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki MilikiĀ©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa