Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amelitaka Shirika la Umeme (TANESCO) mkoani humo kusitisha huduma ya nishati hiyo kwa taasisi ambazo hazilipi madeni zikiwemo za Serikali.
Chalamila ameeleza hayo leo Jumatano Novemba 11, 2020 wakati akizungumza na watumishi wa shirika hilo na kuelezwa malimbikizo ya madeni kwa taasisi za Serikali kwamba yanakwamisha utendaji wa shirika hilo.
Amesema kutokana na changamoto hiyo, TANESCO wasisubiri hadi kufilisika kwa kushindwa kujiendesha na vyema kuchukua hatua ya kuwasitishia huduma ya umeme wanaowadai.
Chalamila alieleza hayo baada ya kuelezwa na shirika hilo kwamba kuna taasisi za Serikali zinadaiwa lakini hazijalipa madeni.
Chalamila alitumia nafasi hiyo kuwaonya watendaji wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) kuachana na tabia ya kuendekeza rushwa na kusababisha malalamiko kwa wawekezaji wadogo wa viwanda na wananchi.
"Wakati wa kampeni za uchaguzi tumekumbana na changamoto katika umeme wa REA, wananchi wanalalamika wanalipia gharama lakini mita wanachelewesha kufunga na kutakiwa wajiongeze..., sasa jambo hilo sitolifumbia macho uongozi wa TANESCO Mkoa mlifuatilie na kutatua malalamiko "amesema.
Ofisa uhusiano TANESCO Mkoa wa Mbeya, Christina Shocki amesema watayafanyia kazi maagizo hayo na kama kutakuwa na changamoto atawasiliana na TANESCO makao makuu.
"Mkuu nimepokea maelekezo pia tutaboresha huduma kwa wananchi hususani kuondoa kero kwa wawekezaji wa viwanda vidogo kutokana na madai ya kupata umeme hafifu na ucheleshwaji wa mita kwa wateja,"amesema.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki MilikiĀ©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa