Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Zuberi Homera leo amefanya mazungumzo na vyombo mbali mbali vya habari mkoani Mbeya kuhusiana kupinga ukatili wa kijinsia ambapo Tanzania kila mwaka inaadhimisha Siku Kumi na Sita (16) za kimataifa za kupinga Ukatili wa Kijinsia ambayo hufanyika kuanzia tarehe 25 Novemba hadi tarehe 10 Desemba.
Lengo la Maadhimisho haya ni kuongeza ushawishi, kujenga uwezo wa pamoja na kuunganisha nguvu za Asasi za Kijamii katika kuhamasisha, kuelimisha, kukemea na kuchukua hatua kwa pamoja ili kupinga Ukatili wa Kijinsia katika jamii.Kaulimbiu ya mwaka 2022, "Kila Uhai Una Thamani: Tokomeza Mauaji na Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto".
Chimbuko la siku 16 ni mauaji ya kikatili ya wanawake watatu (3) wanaharakati wa kupinga ukatili dhidi ya wanawake yaliyofanywa na utawala wa Kidikteta wa Jamhuri ya Dominica tarehe 25 Novemba, 1990. Ilipofika Novemba, 25 mwaka 1999, Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitenga siku hii kuwa ni siku ya Kimataifa ya kupinga Ukatili dhidi ya wanawake.
Kwa mujibu wa taarifa za Dawati la Jinsia la Polisi katika Mkoa wa Mbeya kwa kipindi cha Januari hadi Octoba 2022 jumla ya makosa ya ukatili wa kijinsia 562 yalitolewa taarifa, Makosa yalioongoza ni kubaka 336, kulawiti 54 na shambulio la kudhuru mwili 35, shambulio la aibu 32 na kutelekeza familia 29.
Jumla ya kesi 189 zilifikishwa mahakamani ambapo kesi 11 watuhumiwa wamefungwa jela maisha, kesi 9 watuhumiwa wamefungwa jela miaka 30, 25 watuhumiwa wamefungwa vifungo mbalimbali na kesi 62 zinaendelea mahakamani. Jumla ya kesi 82 hazikuwa na mafanikio.
Aidha jumla ya kesi 136 zinaendelea na upelelezi na kesi 75 zimefungwa polisi kwa kukosa ushahidi.
Wahanga wa ukatili wa kijinsia waliofika katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya kuanzia Januari hadi Oktoba, 2022 kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali ni 4,507 kati yao wanaume 514 na wanawake ni 3,993. Aidha, wahanga waliofika kituoni ndani ya saa sabini na mbili (72) ni 1,464 sawa na asilimia 32.5 ambayo ni ndogo sana, hivyo natoa rai kwa wananchi wote kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za afya pindi wanapofanyiwa ukatili.
Hata hivyo jumla ya watu 1,622 walipimwa VVU, 363 walipata huduma ya kuzuia maambukizi ya VVU (PEP), 255 walipata dawa kinga ya magonjwa ya ngono, 143 walipata dawa ya kuzuia mimba zisizotarajiwa na 2,124 walipata huduma mbalimbali ikiwemo ya kisaikolojia pamoja na rufaa kwenda kwa wadau.
Aidha, Mkoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zina madawati ya Ustawi wa Jamii. Kwa Kipindi cha Januari 2022 hadi Septemba 2022 Mashauri/kesi 1,479 ya ukatili dhidi ya watoto yamehudumiwa, kati ya hayo 1,073 (75%) ni utelekezwaji/kukosa matunzo na mahitaji, 226 (15%) ni ubakaji/ulawiti na 180 (12%) ni ukatili wa kimwili ikihusisha vipigo, kuchomwa moto n.k.
Aidha kumekuwa na sababu mbalimbali zinazopelekea watoto kufanyiwa vitendo vya ukatili katika familia,ikiwa ni pamoja na Migogoro ya familia ambapo jumla ya mashauri 584 sawa na asilimia , Ukosefu wa elimu ya malezi bora jumla ya mashauri 213, Wazazi kutengana au kutalakiana jumla ya mashauri 167, Ndoa za Mitala Jumla ya mashauri (41), Umaskini jumla ya mashauri (34), na Ulevi kwa wazazi/walezi jumla ya mashauri (21)
Changamoto kubwa inayokwamisha mapambano dhidi ya ukatili ni Ushirikiano mdogo kutoka kwa jamii hususani baada ya kufungua kesi, Usiri wa kuficha maovu hasa yanayofanywa na mwanafamilia , pia mwamko mdogo wa wanaume kutoa taarifa za ukatili wanaofanyiwa.
Mkoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na SMAUJATA, Jeshi la Polisi, vyombo vya habari pamoja na wadau mbalimbali tunatekeleza mikakati mbalimbali ya kupinga na kutokomeza Ukatili ikiwemo uanzishwaji wa kamati za ulinzi na usalama za wanawake na watoto ngazi zote za jamii (MTAKUWWA) kutekeleza na kusimamia Afua mbalimbali za kutoa elimu ngazi ya jamii kwa njia za vikundi vya malezi chanya na wawezeshaji ngazi za jamii. Pia kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi dawati la Jinsia kuwafikisha Mahakamani wale wote wanaokutwa na makosa pamoja na kutoa elimu kwa njia ya radio zetu za ndani.
"Wito wangu kwenu, wadau mbalimbali wanaofanya kazi katika Mkoa wa Mbeya zikiwemo Taasisi za dini, Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, Viongozi wa mila, SMAUJATA na wananchi kwa ujumla tuendelee kukemea na kutoa elimu ya kujenga Ari ya kupambana na vitendo vya ukatili. Aidha, Jeshi la Polisi na Mahakama viendelee kuwachukulia hatua wale wote wanaokutwa na hatia ya kufanya vitendo vya ukatili wa Kijinsia" alisema Mhe. Homera.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki MilikiĀ©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa