Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya Rodrick Mpogolo amewataka waandishi na waendesha ofisi za serikali na taasisi mbalimbali za umma na binafsi kuzingatia maadili na kufanya kazi kwa bidii.
Mpogolo amesema hayo wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa waandishi na waendesha ofisi (PS's) mkoa wa Mbeya mkutano uliofanyika katika mji mdogo wa Mbalizi wilaya na mkoa wa Mbeya.
Katibu tawala mkoa wa Mbeya Rodrick Mpogolo ambaye ndiye mkuu wa watumishi wa umma mkoa akiwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo, amesema watumishi hao wasaidizi katika ofisi ni kundi muhimu katika kuleta ufanisi wa kazi.
Amewataka kuendelea kuzingatia nidhamu, bidii na sheria zinazowataka ili kutunza siri za ofisi zao kwa maendeleo ya taasisi husika na serikali kwa ujumla.
Pamoja na kusisitiza utunzaji siri za ofisi pia amewataka kutofumbia macho siri mbaya ndani ya ofisi badala yake watoe taarifa kwenye mamlaka zao za juu ili kutoharibu maadili ya utumishi wa umma.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mbeya Gideon Mapunda, amewataka wataalamu hao kuendelea kushikamana kufanya kazi kwa bidii na kujiona wa thamani ofisini katika kuleta ufanisi na kuchochea maendeleo.
Naye Mwakilishi wa wataalam hao kutoka mkoa wa Mbeya kwenda Taifa Frank Kilomo akitoa taarifa yake, amesema kumekuwa na ongezeko la wajumbe kwenye umoja wa waandishi waendesha ofisi na kuiomba Serikali kupitia waajiri wao kuwajali watumishi hao kwa kuwapa mafunzo ya ndani na nje na kuchochea ari kazini.
Katika mkutano huo wa mwaka wa waandishi na waendesha ofisi (PS's) kutoka ofisi mbalimbali wamekutana kwa lengo la kutafakari ufanisi na changamoto zinazowakabili sanjari na kuchukua hatua za pamoja katika kuendelea kufanya kazi kwa weledi ambapo watoa mada mbalimbali wamefundisha mambo kadha wa kadha ikiwamo wataalam hao kuendelea kuzingatia maadili ya taaluma yao na kuepuka upendeleo kazini ili kuleta usawa.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki MilikiĀ©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa