TAARIFA YA MAENDELEO YA SHUGHULI ZA KILIMO MSIMU WA 2017/2018
1.0 Utangulizi
Mkoa wa Mbeya umeendelea kusimamia shughuli za kilimo kwa msimu wa 2017/2018 kwa kutilia mkazo matumizi ya pembejeo na technolojia mbalimbali za kilimo. Ambapo kwenye maandalizi ya msimu wa kilimo 2017/2018, Tarehe. 23 Oktoba, 2017 Mkuu wa Mkoa aliitisha kikao cha kazi kilicho washirikisha Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa idara ya kilimo na mifugo wa Halmashauri na Maafisa Ugani ngazi ya Kata. Kwenye kikao hicho maagizo mbalimbali yalitolewa yenye lengo la kujipanga kutekeleza kilimo kwa ufanisi. Hii ni pamoja na kubadili fikra, kuweka malengo ya msimu wa kilimo, matumizi ya daftari la kilimo na miongozo mbalimbali ya kilimo na kuboresha huduma za ugani kwa mkulima.
Aidha Mkuu wa Mkoa aliitisha ziara ya mafunzo kwenye Chuo cha Kilimo na Kituo cha Utafiti Uyole ambapo Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na Wataalamu wa Kilimo na Mifugo wa Wilaya walijengewa uwezo na kuagizwa watumie vizuri ujuzi wa kilimo uliyopo kwenye taasisi ya Uyole kwa ajili ya mapinduzi ya Kilimo.
Msimu wa kilimo wa 2017/2018 Mkoa umeweka mkazo zaidi katika kuongeza matumizi ya teknolojia za uzalishaji kwa kushirikiana na taasisi za utafiti na mafunzo, kushirikisha sekta binafsi katika kuendeleza kilimo, kuongeza matumizi ya zana bora za kilimo na kujenga miundominu ya umwagiliaji na maghala ya hifadhi.
2.0 Utekelezaji wa Malengo ya Kilimo
Lengo la Mkoa kwa msimu wa 2017/2018 ni kuzalisha tani 3,939,949 kwenye eneo la hekta 559,589 za mazao ya chakula na tani 118,224 za mazao ya biashara kwenye eneo la hekta 88,304. Vipaumbele katika utekelezaji ni kuongeza tija ya uzalishaji kwa kutumia pembejeo bora za kilimo, kuimarisha udhibiti wa visumbufu vya mazao na mimea, kuendelea kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vya kusindika mazao na kuwaunganisha wakulima na mifumo ya masoko.
Hadi kufikia mwisho wa mwezi wa Januari hekta zipatazo 351,265.69 sawa na 66.7% zimepandwa mazao ya chakula ambapo kati ya hizo hekta 50,936.70 zimepandwa mazao ya kudumu na hekta 300,328.99 zimepandwa mazao ya msimu. Maeneo yanayoendelea kulimwa ni kwa ajili ya mazao ya msimu ikiwemo mpunga, mikunde, mbogamboga na matunda.
Hali ya mvua ni ya kuridhisha; mvua zinaendelea kunyesha kwa wastani na kwa wingi ukanda wa juu, hivyo hali hii ikiendelea kuwepo mavuno yanatarajiwa kuwa ya kuridhisha.
3.0 Pembejeo
Mahitaji ya pembejeo ni pamoja na tani 106,284 za mbolea, tani 89,873.6 za mbegu, tani 95,082 za viuatilifu vya bisi na lita 498,403 za viuatilifu vya kimiminika. Pembejeo hizi zinapatikana mkoani kupitia makampuni makubwa ya pembejeo zikiwemo TFC, DRTC, MeTL, ETG, YARA, PREMIUM, SEEDCO, HIGHLAND SEED Co. na kuuzwa kwenye maduka ya pembejeo mkoani, kwenye Wilaya, Kata na vijijini kupitia mawakala. Kwa ujumla hali ya upatikanaji wa pembejeo hizi ni ya kuridhisha isipokuwa Mbolea ya kukuzia aina ya Urea ambayo imepatikana kwa kuchelewa kidogo. Mkoa unaendelea kuhamasisha makampuni na mawakala wa pembejeo kufikisha pembejeo hizo kwa wakulima haraka. Aidha maafisa ugani wananaendelea kufuatiliwa ili waendelee kuhamasisha wakulima kuandaa mashamba na kutumia kanuni bora za kilimo ikiwemo, kupanda mapema na matumizi mazuri ya pembejeo za kilimo.
Msimu wa 2017/2018 bei ya pembejeo za kilimo zimekuwa zikiendelea kupangwa na makampuni kulingana na soko isipokuwa kwa mbolea ya Urea na DAP ambapo Mkoa umeendelea kutekeleza agizo la kutumia bei elekezi iliyotolewa na TFRA. Aidha kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza kwenye matumizi ya bei elekezi Mkoa umetekeleza maagizo yaliyotolewa na serikali kupitia barua Kumb Na. AC 209/122/01 ya tarehe 24 Januari 2018 iliyoagiza kufanyike mapitio ya bei elekezi ya mbolea kwa kuzingatia umbali wa usafirishaji. Mkoa umetekeleza agizo hilo ambapo bei halisi ya DAP ni kati ya shilling 55,000 – 58,000 ukilinganisha na bei elekezi ya 53,247 – 55,268 na kwa upande wa Urea ni 43,000 – 48,020 ukilinganisha na bei elekezi ya 40,044 – 42,689. Mchanganuo wa mapendekezo ya bei mpya ya pembejeo kwa kila halmashauri ni ifuatavyo;
Jedwali Na. 1. Bei Elekezi na Bei Halisi za Mbolea za DAP na Urea
Na.
|
Halmashauri
|
Bei ya Mbolea (DAP) |
Bei ya Mbolea (UREA) |
||
ELEKEZI |
HALISI |
ELEKEZI |
HALISI |
||
1
|
Busokelo
|
55,268.00 |
56,000.00 |
42,689.00 |
46,000.00 |
2
|
Chunya
|
54,025.00 |
58,000.00 |
41,446.00 |
48,020.00 |
3
|
Kyela
|
54,289.00 |
56,400.00 |
41,710.00 |
44,000.00 |
4
|
Mbarali
|
53,247.00 |
55,000.00 |
40,373.00 |
43,000.00 |
5
|
Mbeya Jiji
|
54,086.00 |
55,500.00 |
40,044.00 |
43,500.00 |
6
|
Mbeya
|
53,640.00 |
56,500.00 |
41,061.00 |
45,500.00 |
7
|
Rungwe
|
54,003.00 |
56,000.00 |
41,424.00 |
46,000.00 |
Chanzo: TFRA & LGAs Desemba, 2017
4.0 Miradi Maalum ya Kilimo
Katika msimu wa 2017/2018, Mkoa wa Mbeya unatekeleza Mpango wa Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), mpango wa kuendeleza kilimo cha zao la Korosho na Programu ya kuendeleza mazao ya bustani.
4.1 Mpango wa SAGCOT
Mpango wa Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (Southern Agriculture Growth Corridor of Tanzania, SAGCOT) ni mpango unaotekelezwa kwa utaratibu wa Kongani (cluster) kwa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi. Utaratibu huu unawezesha wakulima wadogo na wakubwa pamoja na wadau wengine kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuleta ufanisi na faida. Uzinduzi wa Kongani ya Mbarali inayohusisha Mkoa wa Mbeya na Songwe ulifanyika tarehe 27 Oktoba, 2017.
Kazi inayoendelea ni kutambua wadau wa sekta ya kilimo waliopo katika Mkoa, kuchambua fursa za kukuza kilimo na kuzitangaza kwa wawekezaji.
4.2 Mpango wa kuendeleza zao la Korosho
Korosho ni miongoni mwa mazao makuu ya biashara katika Mkoa. Katika kipindi cha mwezi Machi, 2017, zao hili Kitaifa lilichukua nafasi ya kwanza kwa thamani ya mauzo ya mazao nje ya nchi. Kwa sasa zao hili hulimwa kwa kiasi kidogo katika Wilaya ya Kyela.
Pamoja na zao hilo kuwa sehemu ya mhimili mkubwa wa uchumi wa Mkoa, bado uzalishaji wake umekuwa ukikabiliwa na vikwazo vingi ukiwamo ukosefu wa pembejeo, wakulima kutokuwa na teknolojia bora ya uzalishaji hali inayowalazimu wazalishe zao hilo kwa mazoea, hivyo kuathiri maendeleo yake.
Kutokana na hali hiyo, Mkoa wa Mbeya umeona haja ya kuendeleza zao hili kibiashara kwa kupanua kilimo cha zao hilo katika Wilaya za Mbarali na Chunya.
Kuanzia msimu wa 2017/2018 Wilaya za Kyela, Chunya na Mbarali zitaotesha miche ya 132,440 itakayopandwa katika eneo la hekta 1,892. Mkoa umepata mbegu kilo 946, viriba vyeusi kilo 249 na matandazo kilo 78 kwa lengo hilo.
4.3 Programu ya kuendeleza mazao ya bustani
Mkoa wa Mbeya unayo fursa kubwa ya kuzalisha kwa tija mazao ya bustani yanajumuisha matunda, mbogamboga, maua na viungo. Utekelezaji wa Programu ya kuendeleza kilimo cha mazao haya unafanywa na Mkoa kwa kushirikiana na TAHA na wadau wengine. Baadhi ya wadau walioanza kuendeleza mazao ya bustani ni Rungwe Avocado Company, Rungwe Mission, Kuza Africa na Fintrac. Mradi wa Mbogamboga na Matunda unaofadhiliwa na USAID Feed the Future unatekelezwa katika Wilaya za Mbarali, Rungwe na Mbeya. Hadi sasa, chini ya mradi huu vikundi 60 vyenye jumla ya wakulima 2,267 vimepatiwa mafunzo ya mbinu bora za uzalishaji, masoko na lishe.
Kazi inayoendelea ni kujenga miundombinu ya kuhifadhi mazao, kuanzisha vikundi imara vya wazalishaji na kuwaunganisha na masoko.
5.0 HITIMISHO
Mkoa unaendelea kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha inasimamia ukuaji wa kilimo ili kupata chakula cha kutosha na ziada. Hii ni pamoja na kuendelea kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ili kuchochea ukuaji wa sekta ya kilimo. Vilevile ukuaji wa kilimo utatoa fursa ya ajira kwa makundi yote ya jamii na kuchangia malighafi ya viwanda. Vijana na wanawake wanaendelea kuhamasishwa na kujengewa mazingira mazuri ya kujiajiri katika kilimo.
Mkoa unaendela kuwahiza maafisa ugani kutoa elimu kwa wakulima ikiwemo elimu ya matumizi bora ya pembejeo mbalimbali ikiwemo pembejeo za asili na pembejeo za viwandani.
Mkoa unaendelea kuimarisha na kuhamasisha vyama vya ushirika ili kuvijengea uwezo wa kifedha kupitia taasisi za kifedha.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa