Jiji la Mbeya limetoa kiasi cha Shilingi 269,501,500.00 kwa makundi matatu ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2020/2021
Fedha hizo zimetolewa kwa vikundi 32 vilivyokidhi vigezo vya kupatiwa mkopo katika robo hii ya pili, ambapo kati ya hivyo vikundi vya wananwake 22 vimepatiwa jumla ya fedha kiasi cha Shilingi 169,000,000.00, vijana vikundi 7 vimepatiwa jumla ya Shilingi 75,000,000.00 na watu wenye ulemavu vikundi 3 na wenyewe wamepatiwa kiasi cha Shilingi 25,000,000.00
Akisoma taarifa ya Mikopo hiyo Afisa Maendeleo ya jamii wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya ndugu Vincent Msolla aliwaeleza wananchi waliohudhuria hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya kuwa lengo kuu la kutoa mikopo hiyo ni kuwaimarisha wananchi kiuchumi na kuongeza kipato kwa wananchi wasio na ajira
Nae Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya Bwana Amede Ng’wanidako alieleza kuwa Mikopo hiyo iliyotolewa na ofisi yake ni moja ya utekelezaji wa sera za nchi kwa kutoa sehemu ya asilimia kumi ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwaajili ya kuwakopesha makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa uwiano wa asilimia 4 kwa wanawake, asilimia 4 kwa vijana na asilimia 2 kwa watu wenye ulemavu
Akikabidhi Mikopo hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mheshimiwa Albert Chalamila aliwataka wanufaika wa Mikopo hiyo kurejesha kwa wakati mikopo yao ili iweze kuwanufaisha wananchi wengine” Hela hizi sio hisani ni hela za serikali hivyo ni vyema ukipewa mkopo huu ukarejesha kwa wakati ili na wengine wapate kunufaika” alieleza RC Chalamila
Aidha RC Chalamila amewataka wanufaika hao kutumia Fedha hizo kwa shughuli za kibiashara na si vinginevyo, hizi sio fedha za mchango wa harusi au msiba aliongeza RC Chalamila
Akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya Mheshimiwa Dormohamed Issa Rahmat alimhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kuwa atatembelea vikundi vyote vilivyopatiwa Mkopo ili kuweza kuona maendeleo ya vikundi hivyo
Hii ni awamu ya pili ya utoaji wa Mikopo kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021 huku awamu ya kwanza Halmashauri ya Jiji la Mbeya ikitoa Mikopo yenye thamani ya Shilingi 260,000,000.00 kwa vikundi 27 ambavyo vikundi vya wanawake vilikuwa vikundi 15, vijana 6 na vikundi vya watu wenye ulemavu 6
Mpaka sasa katika kipindi cha robo ya kwanza na ya pili, tayari Halmashauri imeshatoa kiasi cha Shilingi 529,501,500.00
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa