ALIYEKUWA Tabibu wa Zahanati ya Uturo iliyopo katika Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, Wilson Chotamganga, ameeleza siri iliyoifanya zahanati hiyo kuwa ya mfano nchini kwa kuzuia vifo vya mama na mtoto kwa miaka 20.
Tabibu huyo ni yule aliyepewa tuzo maalumu ya kutambua mchango wake kwenye kukabiliana na vifo vya mama na mtoto Ikulu jijini Dar es salaam na Rais, Dk. John Magufuli, wakati alipokuwa anazungumza na madaktari.
Akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Mbeya jana katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Chotamganga alisema kuna siri kubwa ambayo aliikuta katika vijiji vinavyohudumiwa na zahanati hiyo ikiwemo ya kuzika ndani watoto waliozaliwa wakiwa wamefariki maarufu kwa jina la ‘sio riziki’.
Alisema mara ya kwanza wakati anafika katika zahanati hiyo mwaka 1993 alikuta kuna msiba wa mwanamke ambaye alifariki wakati anajifungua kwa mganga wa jadi na alipofuatilia zaidi alibaini kuwa mwanamke huyo alikuwa wa tatu ndani ya kipindi kifupi.
Alisema aliendelea kufuatilia na kubaini kuwa kulikuwa na vifo vingi vya mama na mtoto na hivyo akaamua kuanza kuchukua hatua za kukabiliana na vifo hivyo kwa kuwashirikisha wananchi wa maeneo yote ya vijiji.
“Nilikuwa vile vifo vya watoto wachanga na akina mama wajawazito vilikuwa vinasababishwa na nini? Walikuwa wanakufa kwa sababu ya kung’atwa na papasi ama kwa sababu ya marelia? Nilichobaini ni kwamba wengi walikuwa wanajifungulia nyumbani na kwa wakunga wa jadi,” alisema Chotamganga.
Alisema baada ya kubaini mazingira hayo aliamua kuanza kutoa elimu kwa wananchi kupitia mikutano mbalimbali ya vijiji kuhusu umuhimu wa kujifungulia kwenye vituo vya afya na kuachana na wakunga wa jadi.
Chotamganga alisema wananchi wa vijiji hivyo waliaelewa na wakaungana naye kukabiliana na vifo hivyo kwa kuunda kamati maalumu ya wanawake makomandoo ambao walikuwa wanafuatilia afya za wajawazito wote.
“Tuliweka utaratibu wa kila mwanamke akibainika kuwa ni mjamzito, yeye na mwenza wake, wanachukuliwa na makomandoo wanaandikiwa ujumbe wanakuja zahanati kwa pamoja kwa ajili ya kufungua kadi na kupewa elimu,” alisema Chotamganga.
Aliongeza kuwa waliweka adhabu ya sh. 50,000 kwa mwanamke yeyote ambaye atajifungulia nyumbani ama kwa mkunga wa jadi na faini y ash. 5000 kwa mjamzito ambaye hahudhurii kiliniki hali ambayo iliwalazimu wote kujifungulia kwenye zahanati hiyo ya Uturo.
Alisema baada ya kutekelezwa vizuri kwa sheria hiyo ndogo hakujawahi kutokea kifo cha mama na mtoto tangu mwaka 1999 mpaka sasa na kwamba waliokuwa wakunga wa jadi ndio waliokuwa wanaongoza kuwahamasisha wajawazito kwenda zahanati.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Mariamu Mtunguja, alimpongeza Chotamganga kwa utendaji kazi wake na kwamba sifa ambayo Zahanati ya Uturo imepata kwa sasa ni sifa ya mkoa mzima wa Mbeya.
Alisema kwa sasa Serikali inafanya mipango ya kuandaa muundo maalumu wa kukabiliana na vifo vya mama na mtoto kwa kutumia utaratibu wa Uturo ambao utakuwa unatumika nchi nzima.
“Nakuhakikishia kuwa kabla muundo huu haujaanza kutumika maeneo mengine nchini, sisi tutakuwa tumeshaanza kuutumia katika maeneo yote ya vituo vya kutolea huduma ili kuonyesha uhalisia wa muundo,” alisema Mtunguja.
Aliwataka watumishi wengine wa afya katika Mkoa huo kuiga mfano wa Chotamganga kwenye utoaji wa huduma kwa wananchi ili kuokoa maisha ya wananchi
Nebart Msokwa
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa