MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu, awataka viongozi wa Mkoa wa Mbeya kuendana na kasi Serikali ya awamu ya tano ili kufikia malengo yake ya kufikia uchumi wa kati na kwamba viongozi ndio wenye uwezo wa kuwaonyesha wananchi njia sahihi ya maendeleo.
Samia aliyasema hayo juzi jijini Mbeya, baada ya kupokea taarifa ya mkoa huo iliyowasilishwa na Mkuu wa mkoa, Amos Makalla, ambapo alisema ili wananchi wapate maendeleo ni lazima wapate viongozi bora na wachapakazi
Mama Samia amewataka wananchi wa Mbeya kutumia Uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa mwakani kuchagua viongozi wenye fikra za maendeleo na wachapakazi ili kuendana na kasi ya Serikali iliyopo madarakani.
“Nitumie nafasi hii kuwashauri wananchi wa mkoa wa mbeya, katika uchaguzi wa viongozi wetu wa serikali za mitaa, mkatuchagulie viongozi wachapakazi na wenye maono ambao mna uhakika wataendana na kasi ya serikali yetu inayotaka maendeleo,” alisema Samia.
Akisoma Taarifa ya Mkoa wa Mbeya Mkuu wa Mkoa Mh Makalla alisema wananchi wa mkoa huo kwa sasa hawafanyi siasa kama ilivyokuwa miaka ya nyuma na badala yake wanafanya kazi kwa nguvu ili kujiletea maendeleo.
Makalla alisema kuwa wananchi hao wamekuwa wakishiriki shughuli mbalimbali za maendeleo kwa ushirikiano bila kujali tofauti za itikadi za kisiasa hali iliyoufanya mkoa huo kufanya vizuri kwenye miradi mbalimbali inayopelekwa na serikali.
Alisema mkoa huo kwa sasa umeshika nafasi ya nne katika uchangiaji wa pato la taifa ukitanguliwa na mikoa ya Dar es salaam, Mwanza na Shinyanga na kwamba unachangia asilimia 5.3.
“Wananchi kwa sasa wameweka pembeni siasa wanachapa kazi, wananchi hawa hawasukumwi kufanya kazi, ukiwashirikisha suala lolote la maendeleo wanaitikia vizuri ndio maana sisi ukiambiwa kituo cha afya kinajengwa, wananchi wanajitokeza kuchangia,” alisema Makalla.
Aidha alisema changamoto kubwa inayoukabili mkoa huo ni takwimu za maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), kuwa juu kuliko kile kiwango cha kitaifa.
Alisema maambukizi ya Ukimwi katika mkoa huo ni asilimia 9.3 huku kitaifa ikiwa asilimia 4.7 na kwamba mkoa huo ni wa tatu baada ya Njombe na Iringa hivyo akasisitiza kuwa hiyo sio sifa nzuri.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Mbeya, Jacob Mwakasole, alisema chama hicho kinaridhishwa na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015 unaofanywa na viongozi wa serikali.
Alisema utekelezaji huo unawafanya wananchi mkoani humo kuanza kukiamini chama hicho kuliko ilivyokuwa awali ambapo wengi walikuwa wanaonekana kuwa ni wapinzani.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa