Na Nebart Msokwa, MBEYA
SERIKALI mkoani Mbeya, imetangaza kuwa haina mpango wa kuwaondoa wapiga debe kwenye vituo vyote vya mabasi mkoani humo na badala yake itaweka utaratibu mzuri wa kuitambua shughuli hiyo kuwa ajira rasmi kwa vijana.
Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, wakati alipokuwa anazungumza na wapigadebe, makondakta na madereva wa daladala katika kituo cha mabasi cha Nane Nane jijini Mbeya.
Chalamila alisema serikali inakusudia kurasimisha shughuli hiyo kwa kuandaa utaratibu wa kundi la vijana wanaofanya shughuli hiyo kutambuliwa, kuandaliwa sare maalumu na kuwa na vitambulisho kama ilivyo kwa madereva na makondakta.
Aliwataka vijana hao kuwa walinzi wa amani katika maeneo hayo ikiwa ni pamoja na kukomesha vitendo vya udokozi wa mali za abiria na kwamba wao ndio watakaokuwa wanawashughulikia wezi na waharifu wengine kwenye maeneo yao ya kazi.
“Kwa muda mrefu imekuwa ikitangazwa kuwa serikali ina mpango wa kuwaondoa wapiga debe kwenye vituo vyote vya mabasi hapa nchini, nimekuja kuwatangazia rasmi kuwa hakuna atakayewaondoa, hii ni ajira kama ajira zingine,” alisema Chalamila.
Alilitaka kundi hilo kuwa mstari wa mbele katika kusimamia na kufuata sheria ili waendelee kufanya kazi hiyo kwa amani na utulivu pamoja na kushirikiana na Jeshi la Polisi kusimamia amani.
Baadhi ya vijana wanaofanya shughuli hiyo, waliishukuru Serikali kwa uamuzi huo huku wakiziomba halmashauri kuboresha baadhi ya huduma kwenye maeneo yao ya kazi vikiwemo vyoo ili kulinda mazingira.
Mmoja wa wapiga debe hao, Michael Mwanjobe, ambaye anafanya kazi katika kituo cha nane nane alisema kuwa baadhi ya abiria na watumiaji wa kituo hicho huwa wanalazimika kujisaidia kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kutokana na choo cha Jiji kilichopo kuchelewa kufunguliwa.
Mwanjobe alisema huduma hiyo ni mhimu katika eneo hilo lenye mkusanyiko mkubwa wa watu ili pamoja na kulinda mazingira lakini pia walinde afya za watu.
“Hapa kuna choo cha jiji lakini kinafunguliwa kwa kuchelewa, tunaomba hawa wenzetu waweke utaratibu mzuri ili huduma kwenye maeneo haya wanayoingiza fedha ziwe bora,” alisema Mwanjobe.
Aidha alipendekeza kuwa kila kituo cha daladala kiwe na sare kwa ajili ya wapiga debe zenye rangi tofauti na kituo kingine ili kuwatofautisha kwa ajili ya kuwatambua kirahisi wakati wa shughuli yoyote.
Nao baadhi ya wasafiri, waliomba wapiga debe hao kuwa na heshima kwenye kazi yao kwa madai kuwa baadhi yao ni wadokozi na hivyo huwafanya wasafiri kukosa amani wanapofika kwenye vituo hivyo.
Mmoja wa wasafiri hao, Betrice Kasendo, alisema mara nyingi wapiga debe huwa wanalazimisha kuwapokea wasafiri mizigo wakidai wanawasaidia lakini wakati mwingine wanatokomea nayo.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa