MKUU wa Mkoa wa Mbeya Albert Chalamila ametoa muda wa wiki tatu kwa uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuandaa mpango kazi utakaoainisha mahitaji mbalimbali ya watoto wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Itiji na kasha kupeleka wa wadau na Serikali ili kusaidia.
Chalamila alitoa maagizo hayo juzi wakati alipofantya ziara ya kutembelea shule hiyo na kuangalia mazingira wanayosoma watoto wenye mahitaji maalumu.
Kulingana na mazingira aliyoyakuta ambayo hakuna vyoo kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum, vifaa vya kujifunzia na eneo la michezo alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, William Ntinika kwa kushirikiana na viongozi wenzake kuandaa andiko ambalo litaainisha mahitaji yote ya muhimu kwa ajili ya kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum ili wasome kwa furaha.
“Nawapongeza walimu kwa kazi nzuri mnayoifanya licha ya kufundisha kwenye mazingira magumu lakini mnapambana, nimeona hakuna vyoo rafiki kwa watoto wenye mahitaji maalum hapo wanatumia vya watoto wa kawaida lazima tuwashirikishe wadau kusaidia ujenzi huo” alisema Chalamila.
Alisema shule ya Msingi Itiji ni miongoni mwa shule jumuishi ambao zinakabiliwa na vikwazo mbalimbali ikiwemo miundombinu ya madarasa, vyoo, vitendea kazi na maeneo ya michezo.
Aidha alishauri uongozi wa shule hiyo kufanya mawasiliano na walimu wa Shule ya Msingi Makalala iliyopo mjini Mufindi mkoani Iringa kujifunza namna walivyofanikiwa kuendesha shule hiyo yenye watoto wenye mahitaji maalum na kawaida.
Aliwaagiza viongozi wa Jiji kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa bweni ili kuwasaidia watoto wenye ulemavu ambao wanatoka mbali kukaa shuleni na kupunguza tatizo la utoro pamoja na madhara mengine ambayo yanaweza kutokea wakati wa kwenda na kutosha shuleni.
Kutokana na mazingira hayo, Chalamila alitoa msaada wa fedha kiasi cha shilingi milioni moja kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vyoo huku akiwaagiza viongozi wengine kuchangia ili kukamilisha ujenzi wa matundu sita ya vyoo pamoja na ujenzi wa hosteli kwa ajili ya watoto hao.
Akizungumzia tatizo ya uhaba wa matundu ya vyoo kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Jerome Kayange alisema jumla ya watoto 92 wanasoma hapo na kwamba kati ya hao 574 ni watoto wa kawaida.
Alisema shule hiyo ni jumuishi na kwamba miundombinu iliyopo ni rafiki kwa watoto wa kawaida, aliiomba Serikali na wadau wengine kuendelea kuwasaidia ili watoto kusoma katika hali ya utulivu.
Alisema shule hiyo ina jumla ya walimu 20 na kwamba kati yao wanawake ni 17 na wanaume watatu kati yao walimu tisa wakifundisha watoto wenye mahitaji maalum.
Mwalimu anayefundisha watoto wenye matatizo ya akili, Clement Nyabumbwe alisema vifaa vya kujifunzia havikidhi mahitaji kwa madai kuwa watoto wenye shida hiyo muda mwingi wanahitaji shughuli za kufanya na michezo mbalimbali.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa