Hayo yamesemwa na mjumbe wa Kamati Maalumu ya Uelimishaji Wananchi Juu ya Umuhimu wa Uhifadhi na Ujirani Mwema, Afisa Mipango Miji Kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Ndg. Enock Kyando alipokuwa akiwasilisha mada yake ya matumizi bora ya Ardhi katika vijiji vya Uturo, Mtamba, Ukwama na Kapunga Wilaya ya Mbarali siku ya tarehe 07/03/2020.
Kyando alisema kuwa wanakijiji wanapaswa kuzisimamia Serikali zao za kijiji ili ardhi yao isichukuliwe bila kufuata utaratibu kwani kuna baadhi ya sehemu baadhi ya viongozi wamekuwa sio waaminifu wanagawa ardhi ya kijiji bila kuwashirikisha wenye ardhi yao.
*“Msimamizi mkuu wa ardhi ya Kijiji ni Serikali ya kijiji kupitia mkutano mkuu, mtu yeyote anaehitaji kumiliki ardhi ya kijiji anatakiwa kupitishwa kwenye mkutano mkuu ili apangiwe matumizi ya ardhi aliyoiomba, Mtendaji na Mwenyekiti kazi yao ni kupokea maombi tu, Ardhi ni kitu cha muhimu, tusipoisimamia vizuri tutakuja kupigana wenyewe kwa wenyewe”* alisema Kyando
Kyando aliongeza kuwa kijiji kinatakiwa kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi kwani itaondoa migogoro ya mipaka mbalimbali vilevile ni chombo kinachoonesha ni kiasi gani cha ardhi kilichopo kwa ajili ya shughuli za kijiji kama mifugo, kilimo, makazi, viwanda pamoja na matumizi mengine.
Aliongeza kuwa sambamba na kuwa na matumizi bora ya ardhi ya kijiji ni vizuri kila mtu mwenye kipande cha ardhi akachukua hati yake ya kimila yake ambayo inapatikana ofisi ya kijiji ili awe amemiliki kisheria kwani Hati miliki ya kimila ina hadhi sawa na hati miliki zingine za ardhi.
Aidha, Mjumbe mwingine wa timu ya uelimishaji Afisa Mipango Miji Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Ndg Geofrey Mwaijobele amesema kuwa ardhi haiongezeki bali wanadamu na mifugo ndio vinaongezeka kwa kasi hivyo ni muhimu Serikali za vijiji kuweka kipaumbele mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kuepusha migogoro ya wakulima na wafugaji.
Mwaijobele ameongeza kuwa kama maeneo ya misitu na malisho ya mifugo yamehifadhiwa na kijiji ni vyema kila mwananchi akahusika kuyalinda maeneo hayo.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria kwenye mikutano hiyo wameishukuru timu ya uelimishaji iliyoundwa kwani wameongeza uelewa wa masuala ya uhifadhi, kwani walikuwa wanavunja sheria bila kujiua na kupitia elimu hiyo watawaelimisha na wengine ili kudumisha ujirani mwema na wahifadhi.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa