Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe Amos Makalla ametoa siku 14 kwa Halmashauri za Rungwe, Mbeya Jiji, Kyela na Busokelo kulipa madeni ya cheki hewa za Wafanyakazi bora walizotunukiwa kwenye maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani yaliyofanyika mwaka 2016/2017.
Mhe Makalla ameyasema hayo leo kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Dunia (Mei Mosi) yaliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya Uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine yakiwa na Kauli Mbiu ya “ Unganishwaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii ulenge kuleta tija kwa wafanyakazi”.
“ Natoa siku 14 kwa Halmashauri zote zilizotajwa kurejesha fedha hizo kwa wafanyakazi bora walitunukiwa kwa sababu halmashauri mnapenda kutengeneza madeni yasiokuwa ya lazima. Na siku ya leo sitatoa cheki bila kuwa na fedha taslimu”. Amesema
Mhe Makalla amesema kuwa inasikitisha sana kwa Halmashauri kubwa kama Mbeya Jiji kutokuwa na uwezo wa kuwalipa fedha taslimu wafanyakazi wake bora na kutoa ahadi zisizokuwa na utekelezaji kwa muda mrefu sasa.
Akisoma risala Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha Huduma na Ushauri (TUICO) Kanda za Nyanda za Juu Kusini Merboth Kapinga ametoa malalamiko kwa halmashauri hizo kutoa cheki hewa za wafanyakazi bora katika maadhimisho hayo mwaka 2016/2017.
Kapinga amesema kumekuwepo na utamaduni katika baadhi ya waajiri kuteua wafanyakazi bora katika vitendo mbali mbali na siku ya maadhimisho hawatoi fedha bali maneno matupu na kusababisha kuwafunja moyo wa utendaji na hasa kwa watumishi wanaokaribia kustaafu.
Kapinga amemuomba Mkuu wa Mkoa kukemea jambo hilo lisijirudie tena kwani kuna baadhi ya Halmashauri mpaka leo hawajawalipa wafanyakazi mpaka wamestaafu utumishi wao.
Aidha Mhe. Makalla amewaonya Watumishi wa Serikali kuacha matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili kuendana na kasi ya Serikali ya awamu ya tano ili kuweza kutatua matatizo ya wananchi sehemu za kazi kwa wakati.
Amesema kuwa ipo kasumba ya baadhi ya wafanyakazi wanapoingia maofisini jambo kubwa ni kufungua mitandao ya kijamii bila kujali wananchi wanaosubiria huduma jambo ambalo serikali haikubaliani nalo na kuwataka waajiri kufuatilia kwa ukaribu ili kurejesha nidhamu ya utendaji kazi .
Mhe Makalla amekiri Serikali kutambua changamoto za Wafanyakazi hususani kiwango cha kima cha chini cha mshahara, makato makubwa ya kodi na tozo mbali mbali, upandishwaji wa vyeo na madeni ya watumishi ambapo tayari Serikali imeanza kushulikia changamoto hizo.
Amesema kuwa wakati Serikali ikiangalia na namna ya kuboresha maslahi ya wafanyakazi waajiri watengeneze watengeneze mazingira mazuri na wezezeshi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanajiunga katika mifuko ya kijamii wanayotaka na si kuwachagulia jambo ambalo linawanyima uhuru na haki sehemu za kazi.
Mwenyekiti wa TUICO Mkoa wa Mbeya Bibi Winfrida Mnandi amewahimiza wafanyakazi kazi kwa nidhamu katika maeneo yao ya kazi ili kuhudumia wananchi kwa wakati na bila upendeleo na kuwaasa waajiri kuwa karibu na watumishi wao ili kufuatilia utendaji kazi wao.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa