Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe Albert Chalamila ameziagiza halmashauri zote za Mkoa wa Mbeya kutenga fedha kutoka vyanzo vya ndani ili kuendelea kutekeleza afua VVU na UKIMWI hasa kwa kinga na tiba ili kufikia malengo ya Mkoa ya kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI.
Mhe Chalamila ametoa maagizo hayo leo Disemba 1, 2020 kwenye maadhimisho ya kilele cha Siku ya UKIMWI duniani yaliyofanyika viwanja vya Barafu Kata ya Rujewa Wilaya ya Mbarali na kusema kuwa kunahitajika rasilimali za kutosha hasa kipindi kwa kuwa rasilimali kutoka kwa wadau zimepungua kwa kiasi kikubwa.
Amesema kuwa Ili kuongeza kasi ya kuzuia maambukizi mapya ya VV na hatimaye kutokomeza kabisa maambukizi hayo, Mkoa kwa kushirikiana na wadau wengine, umeamua kutekeleza mikakati ya kuzuia maambukizi mapya ya VVU kwa njia mbalimbali kama: kutoa elimu ya mabadiliko ya tabia, ushauri nasaha na upimaji wa VVU , upimaji binafsi wa VVU, tohara kwa wanaume nk.
Mhe Chalamila amesema kuwa kutokana na takwimu za utafiti wa viashiria vya UKIMWI ya mwaka 2016/17 inaonyesha maambukizi ya VVU ni makubwa kwa kundi la vijana na hasa mabinti wa umri wa kati ya miaka 15-24.
“Kwa kweli tukikaa kimya hali Mbeya ukiangalia hata matukio ya kubaka yameshamili sana jambo ambalo ni kichochoe kwa hali ya kupanda kwa maambukizi na kufikia asilimia 9.3 kimkoa na kufika nafasi ya tatu kitaifa
Akisoma taarifa ya Mkoa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Dkt Salum Manyata amesema kuwa Mkoa wa Mbeya umeshika nafasi ya tatu kitaifa kwa kuwa na asilimia 9.3 ya maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi huku waathirika wakubwa ni wasichana wenye wa chini ya miaka 24 kwa asilimia 70.
Dkt Manyata amesema kuwa sababu kubwa ya kundi kuathika kwa kiwango hicho ni kutokaa na mihemko ya kushiriki tendo la ndoa wakiwa na umri mdogo hususan kwa watu waliowazidi umri.
"Licha ya wasichana pia asilimia 30 ya vijana ni wahanga hivyo kuna kila sababu ya kuwa na mpango mkakati wa pamoja ili kunusuru kundi hilo kwani ni nguvu kazi kwa taifa katika kuelekea uchumi wa viwanda "alisema
Aidha amesema kuwa takwimu zinaonyesha vijana walio katika kundi hilo 200 kwa siku wanambukizwa ukimwi huku kwa mwezi ni 6,000 hivyo ni jukumu la wadau mlioshiriki maadhimisho hayo kutafuta mwarobaini wa pamoja ili kuiweka Tanzania ikiwa Salama.
Mratibu wa tume ya kudhibiti UKIMWI(TACAIDS) Mkoa Emmanuel Petro, alisema kwa kipindi cha Oktoba 2019 mpaka Septemba mwaka huu jumla ya wakazi 217,762 walipima afya ambapo 11,185 walipatikana na maambukizi mapya ya Virusi vya ukimwi.Aidha alisema kwa kipindi hicho wajawazito 81,525 walipimwa ambapo kati ya hao 2,063 walikutwa na maambukizi na kuanza kupatiwa tiba na afya zao zinaendelea vizuri.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa