Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe Juma Homera amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Chunya kuwasimamisha kazi na kuwachukulia hatua Watendaji wa Kata 7 kwa tuhuma za kusababisha upotevu wa zaidi ya sh. Milioni 400 ambazo ni mapato ya ndani ya halmashauri mpaka watakaporudisha fedha hizo.
Mhe Homera ameongea hayo leo tarehe 09 Juni, kwenye kikao cha watumishi wa halmashauri hiyo na kusikitishwa na hali duni ya ukusanyaji wa mapato na upotevu wa mapato hayo kutoka kwa watendaji wa halmashauri
“ Sasa nakuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri kuwasimamisha hawa watendaji wote waliosababisha halmashauri kupata hati yenye mashaka kwa wao kukaa na fedha bila kuzipeleka benki kama utaratibu na kanuni zinavyotaka” Mhe Homera
Amesema kuwa watendaji wa kata kwa kushirikiana na watendaji wanatumia fedha mbichi za halmashauri ambazo hazikupelekwa benki baada ya kukusanywa kutoka maeneo mbalimbali kinyume na kanuni na taratibu za halmashauri hiyo.
Aidha, Akiongea kwenye kikao hicho Katibu Tawala wa Mkoa Dkt Angelina Lutambi amewataka wataalamu hao kufanya kazi kwa weledi wakizingatia taratibu na kanuni za serikali na pia kufanya kazi ya kukusanya mapato kwa kushirikiana kuanzi idara ambazo vina vyanzo vya mapato ili yakusanywe kikamilifu.
“Suala la ukusanyaji wa mapato ni la lazima kwa kuwa Serikali ina majukumu makubwa ya kuwahudumia watumishi, kuhakikisha huduma zote zinatolewa na wananchi wananufaika na pia kuendesha serikali kwa hiyo ni wajibu wetu kuhakikisha tunakusanya mapato kikamilifu” Dkt Lutambi
Dkt Lutambi ameagiza kila Mkuu wa Idara kuhakikisha anapitia vyanzo vyote vilivyopo kwenye Idara yake na kuhakikisha anavisimamia na kukusanya mapato kwa kushirikiana na maafisa mapato wa halmashauri.
Naye Mbunge wa Jimbo la Lupa Masache Kasaka amesema kuwa halmashauri lazima iangalie imekosea wapi kuweza kujua wapi imejikwaa na pia amewataka watumishi wa halmashauri kutimiza wajibu wao kwenye kila Idara katika kusimamia ukusanyaji wa mapato ilituweze kutoka hapa tulipo.\
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa