Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Bibi Mariam Mtunguja amezitaka Halmashauri zote ambazo hazijaingia wala kupata mafunzo kutoka kwenye Mpango wa Uimarishaji wa mifumo ya sekta za umma(PS3) kuhakikisha zinatenga bajeti ili kuingia kwenye mfumo huo.
Bibi Mtunguja ametoa wito huo leo alipokuwa anafungua mafunzo ya Mfumo mpya wa kuandaa mipango na bajeti za Mamlaka ya Serikali za mitaa (PlanRep) na kuimarisha utoaji huduma kwa Wananchi nchini yaliyofanyika katika ukumbi wa Usungilo Jijini Mbeya.
Amesema kuwa kupitia mfumo huo ambao umeboreshwa unakwenda kuondoa changamoto ambazo zilikuwepo kwenye mfumo wa zamani hivyo ni muhimu kwa kila Halmashauri nchini kupata mafunzo haya.
Bibi Mtunguja amesema kuwa kutokana na mabadiliko haya na kurahisishwa kwa teknolojia mfumo mpya wa PlanRep umerahisishwa kwa kufanywa kuwa "Web Based" na utawezesha Halmashauri kuingiza taarifa za mipango na bajeti moja kwa moja kwa njia ya mtandao na kutumwa kwenye mfumo uliopo OR- TAMISEMI.
Naye Mwakilishi wa Mradi wa PS3 Dr. Gemin Mtei amesema kwamba mradi huo unaofadhiliwa na Serikali ya Marekani (USAID) ulipelekwa kwenye mikoa 13 na Halmashauri 93 za Tanzania bara ambapo mfumo huu ni wa Kitaifa na uko kwenye toleo la mfumo wa Kielektroniki ambao unatambulisha teknolojia ya mawasiliano na kufanya upatikanaji wake kuwa rahisi mahali popote na muda wowote.
Dr. Mtei amesema kuwa mafunzo hayo yanatolewa na timu ya Wakufunzi kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Sekretarieti za Mikoa,Wakala wa Serikali Mtandao(eGA) Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Wizara ya Fedha na Mipango,PS3 pamoja na Wizara ya Afya.
Mafunzo hayo yamehudhuriwa na Maafisa Mipango, Wahasibu, Wachumi, Maafisa Tehama na Makatibu wa Afya wa Halmashauri zote kutoka Mikoa minne ya Mbeya, Njombe, Iringa na Songwe.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa