Madiwani wa Halmashauri ya Rungwe wametakiwa kusimamia na kuhakikisha kuwa mapato yote yanayokusanywa kutoka kwenye vyanzo vya ndani na Ruzuku ya Serikali yanatumika katika malengo yaliyokusudiwa.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Albert Chalamila wakati akifungua Kikao cha Baraza la Madiwani kujadili hoja za Ukaguzi na kusema ukusanyaji wa mapato ya ndani ni lazima uendane na nidhamu ya matumizi ya mapato hayo.
Mhe. Chalamila amesema kuwa madiwani wanatakiwa kufanya ufuatailiaji wa mara kwa mara ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao na manunuzi yote ya umma yanayofanyika yana thamani ya fedha iliyotumika.
Amesema madiwani wanalo jukumu la kuhakikisha vyanzo vyote vya mapato vinakusanywa kwa kutumia mfumo wa kieletroniki ili kuziba mianya ya upotevu wa fedha za umma.
“Simamieni uwazi na uwajibikaji wa Watendaji kwa kuwapa wananchi taarifa sahihi za mapato na matumizi ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao kupitia mikutano ya hadhara na mbao za matangazo” Chalamila.
Akimkaribisha Mkuu wa Mkoa,Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya Bibi Mariam Mtunguja amesema kuwa kikao hicho cha kujadili Majibu ya Hoja za Ukaguzi na utekelezaji wa mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kina umuhimu wa pekee kwa maendeleo ya Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe.
Bibi Mtunguja amesema kuwa kupitia kikao hiki wananchi na wadau mbalimbali wa Halmashauri hii watapata fursa ya kusikia na kufuatilia shughuli za maendeleo zinazotekelezwa katika Halmashauri yao.
Amewataka madiwani kuwa na ushirikiano na mshikamano katika kujenga halmashauri yao na kusema kuwa nguvu ya pamoja ndiyo inayoendesha Halmashauri na kusukuma maendeleo ya wananchi.
Naye Ezekiel Mwanyemele Mweneyekiti wa Halmashauri ya Rungwe amempongeza Mkuu wa Mkoa kwa kuteuliwa na kuwahidi kusimamia mapato ya halmashauri hayapotei kizembe ili kuhakikisha miradi iliyopangwa inatekelezwa kwa wakati na kwa ubora.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa