Wafugaji wa mkoani hapa wameambiwa hadi kufikia Novemba 30 mwaka huu wawe wameweka chapa mifugo yao, tofauti na hapo Serikali itachukua hatua kali dhidi yao.
Rai hiyo ilitolewa jana mchana na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla katika kikao cha ndani na wafugaji wa Wilaya ya Mbarali kilichofanyika mjini Rujewa kikihusisha kamati nzima ya ulinzi na usalama ya mkoa huo.
Makalla alisema tangu agizo la wafugaji kupiga chapa mifugo yao kwa ajili ya utambuzi Julai mwaka huu kumekuwa na kasumba ya kusuasua hadi sasa kwani ni ng’ombe 12,000 pekee iliyokwisha wekewa chapa kati ya 200,000 iliyokusudiwa wilayani hapa.
“Tunataka kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi, kudhibiti ufugaji na uingizaji holela wa mifugo kwa kila wilaya ndio maana tunasisitiza mifugo yote ipigwe chapa, lakini zoezi hili linaonekana kusuasua, hivyo basi baada ya Novemba 30, hakutakuwa na msamaria mwema katika hili,”alisema Makalla.
Mbali na hilo, Makalla pia wafugaji kuacha tabia ya kuendelea kuingiza mifugo yao katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha huku akisisitiza kwamba kuanzia sasa mfugaji yoyote atakayekutwa ndani ya hifadhi hiyo hatalipishwa faini kwa kosa ya kuingiza mifugo yake bali mifugo hiyo itataifishwa moja kwa moja na Serikali kupitia mamlaka ya Tanapa.
Alisema ‘Kinachoonekana hapa kulipishwa faini sio shida kwenu wafugaji, leo mnakatwa na kwa kiburi mlipa faini hiyo halafu mnardi tena ndani ya hifadhi kwani fedha kweni fedha ipo. Sasa basi hili tutalitazama upya…. Mifugo ikikamatwa ndani ya hifadhi hatua ya moja kwa moja ni kutaifisha mifugo yote’.
Hata hivyo wafugaji hao kupitia kwa uongozi wao wa Chama Cha Wafugaji Tanzania (CCWT) Wilaya ya Mbarali, walitoa kilio chao kwa Makalla kwamba wamekuwa wakinyanyasika kutokana na kukosa maeneo ya malisho wala mipaka ya hifadhi ya Ruaha kutoeleweka bayana jambo linalowafanya wakamatwe hovyo na kulipishwa faini zisizostahili kutoka kwa askari wa wanyamapori kwa madai wapo eneo la hifadhi.
Katibu wa CCWT, Wilaya ya Mbarali, Matagiri Mbigiri alisema Wilaya ya Mbarali ina jumla ya wafugaji 8,000 ambao ufugaji ndio shughuli kuu lakini kwa sasa wanaona ufugaji ni shubiri kwao kutokana na kunyanyasika.
Alisema ‘Tupo tayari kutoa ushirikiano wa dhati kwa Serikali kutunza na kuhifadhi hifadhi ya Ruaha. Lakini tunachoomba tutengewe na kuboresha maeneo ya malisho ambayo yatakuwa rafiki kwa mfugaji.
Mkuu wa Wilaya ya ya Mbarali, Reuben Mfune alimhakikishia Makalla kutekeleza yale yote waliyoagizwa huku akiwataka wafaugaji kuendelea kuzingatia elimu ya ufugaji bora ili kuepuka usumbufu usiokuwa na tija kwao.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa