Serikali Mkoa wa Mbeya imeiagiza Halmashauri ya Jiji kuweka utaratibu mzuri wa kuwatambua na kuwasajili wapiga debe na mama lishe wanaofanya shughuli zao eneo la stendi kuu ya mabasi kama wafanyakazi wa eneo hilo ili kuwajengea mazingira mazuri ya kufanya kazi zao.
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mh. Amos Makalla alipokuwa akikabidhiwa jengo la abiria lililofanyiwa ukarabati na halmashauri hiyo kwa kushirikiana na kiwanda cha soda cha Pepsi.
Mhe. Makalla amesema kuwa ni vizuri kuwatambua vijana hao rasmi kwa shughuli wanazozifanya za kujiingizia kipato ili kuondokana na adha wanayoipata ya kukamatwa na askari wa Jeshi la Polisi kila mara wanapokuwa kwenye shughuli zao.
“Halmashauri ya Jiji mnatakiwa mjipange kuwawezesha vijana hawa kuwa na vitambulisho na sare zao hata kwa kuomba kusaidiwa kutoka kwa makampuni mbalimbali yaliyopo hapa kuepusha vijana hawa kurudi mtaani na kuanza shughuli za uvunjifu wa sheria” amesema
Aidha, Mhe. Makalla ameipongeza halmashauri kwa kuweza kutoa fedha kutoka Serikalini na Kata ya Sisimba za ukarabati wa jengo la abiria kama alivyoagiza baada ya awali kulitembelea na kuona jinsi lilivyokuwa limeharibika.
Pia Mhe Makalla amemshukuru Mkurugenzi wa Kiwanda cha Pepsi tawi la Mbeya kwa kuweza kuchangia ukarabati huo kwa kuingiza mfumo wa umeme na kujenga viti kwenye jengo hilo kwa ajili ya abiria.
Awali akisoma taarifa ya ukarabati wa jengo hilo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji Dkt. Amani Kilemile amesema kuwa ukarabati wa jengo hilo umefanywa na mkandarasi Bakanja Investment LTD na ulianza tarehe 31/08/2017 kwa gharama za shilingi 32,117,712/= kutoka ruzuku ya Serikali na shilingi 5,616,300 mchango kutoka Kata ya Sisimba.
Dkt Kilemile amesema kuwa halmashauri imelifanyia ukarabati jengo hilo kwa lengo la kuhakikisha kunakuwepo na usalama wa abiria na mali zao wawapo stendi na kuondokana na adha waliyokuwa wanaipata.
Akitoa changamoto za watumiaji wa stendi hiyo Diwani wa Kata ya Sisimba Mhe. Geofrey Kajigili amelalamikia kutokuwepo na choo bora kwa ajili ya abiria kwani choo kilichopo ni kibovu na hakifai kwa matumizi ya binadamu.
Aidha, Mhe Kajigili ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuhakikisha wanakarabati taa za stendi ambazo zina muda mrefu haziwakiwa na hivyo kuwapa wakati mgumu wafanyabiashara wadogo hasa mama ntilie wanaofanya kazi hadi usiku.
Mhe Kajigili ameiomba halmashauri pia kutoa elimu kwa wafanyabiashara walioambiwa wakarabati vibanda vyao kwa kuwa wamekuwa na wasiwasi wa kupandishiwa bei ya kodi baada ya zoezi hilo.
Ukarabati wa jengo la kusubiria abiria kituo kikuu cha mabasi ulianza tarehe 31/o8/2017 baada ya agizo la Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kwa halmashauri alipotembelea na kuona ubovu wa jengo hilo.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa