Kukamilika kwa utengenezaji wa Meli za Mizigo na abiria katika Bandari ya Itungi kutafungua fursa za kiuchumi na kufungua fursa za kimapato kwa Wananchi na Serikali na kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara kwa kutumia miundombinu ya barabara.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe Amos Makalla wakati Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ilipofanya ukaguzi wa utengenezaji wa Meli tatu mpya za Mizigo na Abiria katika Bandari ya Itungi Wilayani Kyela.
Mhe. Makalla amesema kuwa kukamilika kwa Meli hizo kutasaidia usambazaji wa bidhaa mbalimbali ambazo viwanda vilivyopo Mbeya vinapata shida kuzunguka kupata. Aidha, mradi huu utaunganisha Tanzania na Malawi ambapo nchi ya Malawi inategemea sana usafiri wa Meli kwa ajili ya kusafirishia bidhaa za kutoka na kuingia nchi hiyo.
“ Mahitaji na matumizi ya wananchi ni makubwa mno na Serikali ya Mkoa inataka kuona utengenezaji wa Meli hizi unakamilika kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika mapema na jitihada za Serikali yao”.
Kwa upande wake Meneja wa Bandari Kyela Bw. Ajuaye Msese amesema kuwa mradi wa ujenzi wa Meli unaendelea utarahisisha shughuli za kiuchumi kijamii na kiusalama kwa wanancnhi wa eneo la Bandari. Mamlaka imelenga kuifanya Bandari ya Itungi kuhudumia abiria na Mizigo mchanganyiko na ile ya Kiwira kuhudumia Mizigo kama Makaa ya Mawe, Mbolea na Saruji kama sehemu ya utekelezaji wa sheria ya Mazingira.
Bw. Msese amesema kuwa Mamlaka iko katika hatua nzuri za kuhakikisha inapata eneo katika Mkoa wa Mbeya kwa ajili ya ujenzi wa Bandari Kavu ambayo itakuwa kiungo muhimu kwa Mizigo inayosafirishwa kutoka Dar es Salaam kupitia reli ya TAZARA kwenda nchi jirani Malawi, Zambia na DRC.
Naye Mkuu wa Wilaya wa Kyela Bi. Claudia Kita ameahidi ushirikiano wa kutosha kwa Mamlaka ya Bandari katika kuzuia shughuli za kibinadamu pembezoni mwa Mito ili kuzuia mchanga kujaa katika kingo za ziwa Nyasa
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa