Na Nebart Msokwa, NIPASHE.
MBUNGE wa Jimbo la Mbarali mkoani Mbeya, Haroon Pirmohamed, ametangaza kuwalipia wakulima wadogo wa Wilaya hiyo zaidi ya shilingi milioni 800 wanazodaiwa kwa ajili ya mkopo wa matrekta kwa ajili ya kuendeleza kilimo.
Mbunge huyo alitangaza kubeba mzigo huo juzi wakati wa Ziara ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu, katika Wilaya hiyo ambapo alisema wananchi hao walimuomba awasaidie kwa madai kuwa wameshindwa kulipa deni hilo.
Alisema wananchi hao walikopa vifaa hivyo kwa makubaliano ya kulipa kidogo kidogo kila wanapovuna mpunga lakini kufuatia kukabiliwa na changamoto mbalimbali wameshindwa na hivyo akaona ni vema aubebe mzigo huo.
“Mheshimiwa makamu wa rais, kuna wakulima wenzangu 330 walikopa matrekta na wakadhaminiana wenyewe, sasa deni hilo wameshindwa kulilipa na wamekuwa wakiwakimbia wanaowadai, sasa kuanzia sasa wasimkimbie mtu, nalibeba mwenyewe nitashirikiana na marafiki zangu,” alisema Haroon.
Makamu wa Rais, Samia alimpongeza Mbunge huyo kwa kuwasaidia wananchi hao na akawataka wananchi hao kuuchukulia msaada huo kama deni kwa kiongozi huyo kwa madai kuwa wanatakiwa waje walipe fadhira.
Aliwataka wananchi hao kutobweteka kutokana na msaada wa kiongozi huyo kwa madai kuwa ipo siku atakuja mbunge ambaye hatakuwa na moyo wa kuwasaidia kwenye mambo kama hayo.
Samia alisema wananchi hao wangeweza kulipa deni hilo kwa kulipa kidogo kidogo kila baada ya kuuza mpunga wao wanaolima, badala ya kuanza kutegemea msaada kama huo.
Aliwasisitiza wananchi hao kufanya kazi kwa bidii ili kuinuka kiuchumi na kuwa na uwezo wa kusimama wenyewe kwa miguu yao badala ya kuwa wategemezi.
“Rais wetu anasisitiza kila siku kuwa ‘hapa ni kazi tu!’ sasa nawaomba mchape kazi, msitegemee kulipiwa madeni kama hivi alivyofanya mbunge wenu, ipo siku ataondoka na hamtapata mtu wa kuwasaidia kama hivi, hii ni changamoto kubwa kwenu,” alisema SAMIA.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mchungaji Jacob Mwakasole, alimshukuru mbunge huyo kwa kuwasaidia wananchi hao kwa madai kuwa sio kwamba anawasaidia wakulima hao pekee bali anakisaidia pia chama hicho kuheshimika.
Alisema mbunge huyo mbali na kuamua kubeba deni hilo la wananchi wake, pia amekuwa akiwasaidia vitu vingi ikiwa ni pamoja na kugawa vifaa vya kilimo kama matrekta na kuboresha miundombinu ya elimu na afya.
Alisema kiongozi huyo anawafanya viongozi wa CCM wanapopita katika Wilaya hiyo watembee kifua mbele kwa madai kuwa wanawafanya wananchi wawaheshimu kwa sababu mbunge huyo anatokana na chama chao.
“Pia amekisaidia chama kwa kugawa pikipiki kwenye jumuia zake zote ndani ya wilaya hii kwa ajili ya kuwasaidia wanapofanya shughuli za chama, pia amekuwa akiwasaidia wananchi wake kuwachangia michango ambayo huwa wanatakiwa wachangie kuboresha miundombinu kama ya shule.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa