Mamlaka za Serikali za Mitaa Tanzania zinatarajia kuanza kutumia mfumo mmoja wa uhasibu wa usimamizi wa fedha za umma toleo la 10.2 (Epicor 10.2) utakaoanza kutumika tarehe 1 Julai, 2018 ili kusaidia mfanano katika uhasibu, utoaji taarifa na usimamizi wa fedha.
Akizungumza katika Mafunzo ya Wahasibu na Waweka Hazina wa halmashauri za mikoa ya Mbeya, Songwe na Rukwa Mkuu wa Mfumo wa Mawasiliano PS3 Bw. Desderi Wengaa amesema kuwa uzinduzi wa mfumo huo mpya utafuatiwa na Mafunzo ya kina ya wiki tatu kwa watumishi 950 wa kada za uhasibu kutoka halmashauri 185 za Tanzania Bara.
Bw. Wengaa amesema kuwa Mafunzo hayo yataendeshwa na Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa pamoja na Serikali ya Marekani kupitia mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS 3) katika mikoa ya Mbeya, Dodoma, Iringa, Mtwara, Kagera na Mwanza.
Amesema kuwa moja kati ya maboresha makubwa katika mfumo mpya wa usimamizi wa fedha za umma ni kushushwa kwa mfumo hadi kwenye ngazi ya mtoa huduma ambapo matumizi yote yanayofanywa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa vituo vyake vya afya na shule yatahifadhiwa na kuwekwa wazi kwa vituo vya kutolea huduma pamoja na jamii wanayoitumikia” alisema Afisa huyo.
Bw. Wengaa amesema matoleo yaliyopita ya mfumo wa usimamizi wa fedha za umma yalijumuisha hitilafu za kiufundi ambazo zilididimiza mbinu bora za uhasibu na taratibu za usimamizi wa fedha, na kusababisha kuwepo kwa hati chafu kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Amesema kuwa mfumo wa Epicor 10.2 utaunganishwa na mfumo unaowezesha mabenki kulipana Tanzania (TISS) ambao utaruhusu malipo yote kufanyika kwa njia ya kielektroniki, pia unahusisha Muundo mpya wa uhasibu (New Chart of Account) pamoja na Kasma Mpya ya 2014 (GFS) kama ilivyoelekezwa na Wizara ya Fedha na Mipango.
Akifungua Mafunzo hayo Afias Elimu wa Mkoa Bibi Paulina Ndigeza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa amewapongeza waandaaji wa Mafunzo kwa kufanikisha utengenezaji wa mfumo huo.
Bibi Ndigeza amesema kuwa Mafunzo hayo yana lengo la kuwajengea uwezo ili waweze kusimamia mapato na matumizi ya Fedha za Umma kwenye Halmashauri na pia kuwapatia uelewa wa mabadiliko ya msingi yalilofanyika bila kukwamisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Ameongeza kuwa Mafunzo hayo yataondoa changamoto za utoaji wa taarifa hasa kutoka kwenye vituo vya kutolea huduma pamoja na kuunganisha Taarifa hizo kwenye Hesabu za Halmashauri, pia utatoa taarifa za utekelezaji za mipango na bajeti kwa kuzingatia matumizi ya fedha yaliyofanyika.
Bibi Ndigeza amewapongeza wataalam wote walioshiriki kufanikisha mifumo yetu ya LGRCIS (Mfumo wa Mapato), PlanRep, FFARS na Epicor kuweza kubadilishana Taarifa na kuwashukuru sana Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) kupitia mradi wa PS3 kwa kufadhili Mafunzo.
“Sisi Makatibu Tawala wa Mikoa, ambao ni viongozi wa Mikoa tutahakikisha matumizi sahihi ya mifumo yanakuwepo ikiwemo matumizi ya taarifa katika kufanya maamuzi kuanzia ngazi za vituo vya kutoa huduma mpaka ngazi ya Mkoa” amesema Katibu Tawala.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa