Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Amos Makalla amekabidhi magari mawili kwa Halmashauri ya Jiji la Mbeya yenye thamani ya shilingi 191,703,073 kwa ajili ya kufanya ziara za usimamizi shirikishi na uhakiki wa ubora wa taarifa kwenye masuala ya UKIMWI.
Akikabidhi magari hayo yaliyofadhiliwa na watu wa Marekani kupitia shirika la HJF Medical Research International, Mh. Makalla alieleza furaha yake kwa Serikali ya Marekani kwa kuwa na imani na Mkoa wa Mbeya hadi kufikia hatua ya kutoa msaada katika sekta mbalimbali ikiwemo ya afya.
Mhe. Makalla alisema bajeti ya Marekani imekua ikiongezeka kila mwaka ili kufanikisha mataifa katika masuala mbalimbali ya kijamii ikiwemo utoaji wa huduma bora za afya kama ilivyo kwa Tanzania.
“ Wafadhili wametoa msaada ni lazima Wakurugenzi wasimamie kutunza magari haya ili yaweze kusaidia na kufanya kazi iliyokusudiwa kwa ajili ya mapambano dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi,” alisema Mhe Makalla.
Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji Dkt. Jonas Lulandala alisema magari hayo yatasaidia sana katika ukusanyaji wa sampuli za damu kwa wakati na upelekaji katika maabala ya Kanda, kusambaza dawa na vifaa tiba kwa wakati.
Dkt Lulandala amesema kuwa halmashauri imekuwa ikifanya ziara za usimamizi shirikishi na uhakiki ubora wa taarifa mara kwa mara katika vituo vyote vya huduma ya afya, tiba na matunzo pamoja na ufuatiliaji wa ubora wa kazi kwa watoa huduma na kwendesha mafunzo kazini yaani ‘Mentorship’.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya Mh David Mwashilindi aliahidi kuisimamia Halmashauri yake ili kuyatumia magari hayo kama yalivyokusudiwa.
Mhe. Mwashilindi amesema kuwa Halmashauri ya Jiji la Mbeya inatekeleza mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi katika Mkoa wa Mbeya kwa kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi, upimaji wa VVU, utoaji wa dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi ARVS pamoja na upimaji wa wingi wa virusi vya ukimwi.
Mradi wa HJFMRI umetoa magari 11 kwa Ofisi ya Mkuu wa Mko wa Mbeya na Halmashauri zake kwa lengo la kuwezesha kufanya ziara za usimamizi shirikishi na uhakiki wa ubora wa Taarifa mara mara katika Vituo vyote vya huduma ya afya, tiba na matunzo na pia kwenye ukusanyaji sampuli za damu kwa wakati na upelekaji wa sampuli katika maabara ya Kanda.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa