Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Amos Makalla amezitaka halmashauri za Mkoa kuhakikisha kuwa mipango na Bajeti za halmashauri zao zilenge kupunguza umaskini na kutatua kero za wananchi hasa sehemu za Vijijini.
Mhe. Makalla ameyasema hayo leo wakati wa Kikao cha viongozi na watendaji kupokea taarifa ya viashiria vya umaskini nchini iliyoandaliwa na shirika la utafiti juu ya kupunguza umaskini (REPOA)
Amesema kama umaskini unapimwa kwa hali ya kipato au kumudu huduma za msingi basi ni jukumu la viongozi na watendaji kuweka mipango mizuri kwenye bajeti zao za namna ya kusimamia masuala ya kuwezesha wananchi kiuchumi.
Akitoa wasilisho la viashiria vya umaskini Mtafiti Mwandamizi Dkt Blandina Kilama (Phd) amesema kuwa mwaka 2015 Wizara ya Fedha iliomba REPOA kufanya kazi ya kutafuta viashiria vya umaskini kwa wilaya ambazo zina umaskini na wilaya zenye auheni ya umaskini.
Dkt Kilama alisema utafiti huu umekuja baada ya Taarifa ya awali kulalamikiwa na Wilaya zilizokuwa zina kiwango kikubwa cha umaskini na Wilaya zilizokuwa na kiwango kidogo cha umaskini.
Amesema kuwa kwa Mkoa huu Mbarali ndio imechukuliwa kufanyiwa utafiti baada ya kuonyesha kuna ongezeko kubwa la umaskini toka mwaka 2002 umaskini ulikuwa 13.1% na kufikia mwaka 2012 ilikuwa na kiwango cha 23.6%.
Akichangia wasilisho hilo Afisa maendeleo ya Jamii Chunya Bibi Ester Mwakalindile amesema ni vema kupima viashiria vya umaskini kutokana na rasilimali zilizopo katika eneo husika ili kuweka uhalisia wa Takwimu za umaskini katika halmashauri.
Bibi Mwakalindile amesema kuwa viashiria vya umaskini haviwezi kuwa sawa kila halmashauri nchi ukizingatia kuna tofauti ya hali ya hewa ya eneo kwa ajili ya kilimo, maeneo ya shughuli za kijami, Elimu nan uelewa wa wananchi wa maeneo husika.
Utafiti wa hali ya kipato kwa kaya wa mwaka 2012 ndio umepelekea kuanza kwa utafiti wa viashiria vya umaskini katika baadhi ya mikoa ukiwepo mkoa wa Mbeya hususani Wilaya ya Mbarali.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa