Mkoa wa Mbeya umepanda miti 6,080,667 mwaka 2019/2020 sawa na asilimia 58 ya lengo lililowekwa kimkoa la kupanda miti 10,500,000 kwa mwaka.
Hayo yamesemwa na Ndugu Said Madito, Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kupanda miti kimkoa iliyofanyika Wilaya ya Mbarali na kusema kuwa miti 4,424,092 ilistawi sawa na asilimia 73 ya miti yote iliyopandwa.
Madito amesema kuwa tangu mvua zimeanza kunyesha zaidi ya miti 102,799 imepandwa kwa kushirikiana Viongozi na Wananchi katika halmashauri zote na shughuli hii ya upandaji miti itaendelea kipindi chote cha mvua.
“Kila halmashauri inatakiwa kuweka msukumo wa kutosha wa kuwa na kitalu cha miche isiyopungua 1,500,000 ili kufikia lengo la kupanda na kuwa na ufanisi katika kutekeleza kampeni ya upandaji miti”. Madito
Akisoma hotuba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Mhe Reuben Mfune amewataka viongozi wa serikali kushirikiana na wadau kusimamia ufuatiliaji utunzaji wa miti iliyopandwa kikamilifu pamoja na kupambana na wananchi wanaochoma moto hovyo misitu.
“Naamini kuwa ufuatiliaji imara utasaidia katika kuongeza uzalishaji na kuboresha ustawi wa miti iliyopandwa , aidha, nazitaka kamati za vijiji zinazosimamia mazingira kuongeza ufanisi katika kusimamia upandaji na utunzaji wa miti ili kuweza kupata manufaa”. Mhe Mfune
Naye Mwakilishi wa Meneja wa Misitu Kanda (TFS) Bibi Unice Mbilinyi amesema kuwa tayari wameanzisha bustani kila halmashauri kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali kulinda mazingira katika vyanzo vya maji.
Bibi Mbilinyi amesema TFS pia imepandaa miti kwa ajili ya kuwagawia wananchi na kusema kupanda miti huenda sawa na kutunza mazingira hivyo kuwataka wananchi kuhakikisha wanaitunza miti ambayo wanapanda kwenye mazingira yao.
Kampeni ya upandaji miti ni ya kitaifa ambapo hufanyika nchini kote kwa tarehe tofauti kulingana na misimu wa mvua katika kutekeleza Waraka wa Waziri Mkuu kwa lengo la kupambana nakuenea kwa jangwa na kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi, mkazo ukiwekwa katika kuhifadhi vyanzo vya maji na kuimarisha hifadhi ya mazingira.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa