SERIKALI Mkoani Mbeya imesitisha kuondolewa kwa wakazi wa Kijiji cha Sipa kilichopo katika Kata ya Kambikatoto wilayani Chunya kutokana na mipaka ya eneo la Kijiji hicho kutoeleweka vema iwapo ni sehemu ya hifadhi,pori la akiba au eneo tengefu la malisho.
Hayo yamejiri zikiwa ni siku chache tangu Serikali wilayani Chunya ifanye oparesheni ya kuwaondoa wavamizi wa maeneo ya Hifadhi na mapori ya akiba wilayani hapa ambapo wakazi wa kijiji cha Sipa pia ilikuwa waondolewe kijijini hapo.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini Sipa juzi,Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na Usalama Mkoa wa Mbeya,Mkuu wa Mkoa ,Amosi Makalla aliamuru wakazi hao wapatao zaidi ya 8000 waendelee kuishi kwa amani kijijini kawao.
“Taarifa zenyewe zinajichanganya,wapo wanaosema eneo hili ni la Tanapa,wapo wanaosema ni eneo lilitengwa kwaajili ya malishio ya mifugo ya kijiji mama cha Kambikatoto na wengine wanasema ni pori la akiba.Lakini mpaka mnajenga majengo ya shule,mna mtendaji na mwenyekiti wa kijiji kwa nini leo tuseme mpo hapa kinyume cha sheria”
“Sasa ninachosema mimi kuanzia leo endeleeni kuishi kwa amani katika eneo hili ambalo mmejenga.Lakini nataka viongozi wa kijiji mama cha Kambikatoto walete mihutasari inayoeleza eneo hili lilitengwa kwaajili ya nini ili tuone nini cha kufanya”alisema Makalla.
Hata hivyo Mhe. Makalla aliwaonya watu wote waliotimuliwa kwenye maeneo ya hifadhi yakiwemo ya Mdabulo na Manyanga kutorejea tena huko kwakuwa kuondolewa kwao kuna sababu za msingi kisheria.
Awali mkuu wa wilaya ya Chunya,Rehema Madusa alisema asilimia kubwa ya wakazi wa kijiji cha Sipa ni wahalifu waliokimbia kutoka maeneo mbalimbali nchini hivyo walihamia kwenye eneo hilo kama sehemu ya kujificha lakini wakiwa hapo wamekuwa wakijishughulisha na shughuli mbalimbali za uharifu ikiwemo uwindaji haramu wa Tembo na uvunaji magogo na mbao.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa