Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. A mos Makalla, imeufunga Mgodi mmoja na kusimamisha kiwanda kimoja cha kuchenjua dhahabu wilayani Chunya kutokana na kukiuka taratibu za madini ikiwemo kutumia milipuko mikubwa inayosababisha madhara kwa wananchi.
Mgodi uliofungwa ni wa Gabriel Resources, ambao unadaiwa kusababisha madhara makubwa kwa wananchi wa Kijiji cha Mlima Njiwa katika Kata ya Mbugani kutokana na kutumia milipuko iliyosababisha kubomoka kwa nyumba za wananchi pamoja na Zahanati.
Akitangaza uamuzi wa Kuufunga Mgodi huo kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Mlima Njiwa, Mhe Makalla, alisema alipata malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa wawekezaji hao wanasababisha madhara kwao.
Makalla alisema baada ya kupata malalamiko hayo, alifika katika kijiji hicho na kuwasikiliza wananchi pamoja na mwekezaji wa Mgodi huo ambaye alikiri kutumia milipuko hiyo ndipo akaamua kusimamisha shughuli za uchimbaji na kisha kuunda tume ya kuchunguza tuhuma hizo
“Tulipofanya mkutano hapa mlitoa ushuhuda kuhusu madhara mnayoyapata kutokana na milipuko ambayo ilikuwa inafanywa hata mchana, mlieleza namna nyumba zenu zilivyopata mipasuko na zahanati yenu kubomoka, wanafunzi wanavyopata shida shuleni,”
“Tume imebaini kuwa kweli mwekezaji huyu alikuwa anatumia milipuko mikubwa na hata baada ya mimi kusimamisha shughuli za ulipuaji wao waliendelea kulipua na kuendelea kuleta madhara kwa wananchi, sasa kuanzia sasa naufunga mgodi huu pasifanyike shughuli zozote,” alisema Makalla.
Aidha Makalla alisema waliamua kusimamisha shughuliza uchenjua dhahabu za Kiwanda kinachomilikiwa na Isack Msowoya, kilichopo katika Kijiji hicho cha Mlima Njiwa, kutokana na kujengwa kwenye eneo la chanzo cha maji na hivyo kuhatarisha maisha ya wananchi kutokana na matumizi ya kemikali.
Vilevile alisema mmiliki wa Kiwanda hicho hana kibali chochote cha kumuwezesha kuendelea na shughuli za uchenjuaji wa madini ikiwemo kibali cha Baraza la Mazingira la Taifa (Nemc), Jeshi la Zimamoto pamoja na cha Usalama mahali pa kazi (Osha).
Alisema kitendo cha mwekezaji huyo kutokuwa na vibali hivyo ni kosa kisheria na kwamba kuna uwezekano wa kemikali zinazotumika kuchanganyika kwenye maji wanayotumia wananchi.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji hicho, waliishukuru Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kwa uamuzi wake wa kuufunga Mgodi huo pamoja na Kiwanda kwa madai kuwa walikuwa katika hatari ya kuathirika na shughuli hizo.
Diwani wa Kata ya Mbugani, Bosco Mwanginde, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chunya, alisema uamuzi huo ni mzuri kutokana na wawekezaji hao kubainika kuwa walikuwa wanakiuka sheria za nchi.
Alisema wananchi wake walikuwa wanaathiriwa na shughuli za mgodi pamoja na kiwanda hicho na kwamba endapo shughuli hizo zingeachwa ziendelee, madhara yangekuwa makubwa zaidi.
“Pamoja na kwamba hawa watu walikuwa wanalipa kodi na kuajiri watu wetu, lakini maisha ya watu ni mhimu zaidi kwahiyo, kamati ya ulinzi na usalama imetusaidia sana,” alisema Mwanginde.
Naye Eva Daniel, alisema Serikali imewasaidia kwa madai kuwa Mgodi wa Gabriel Resources, umesababisha madhara kwao kwa kubomoa nyumba na kwamba walikuwa wanaishi kwa wasiwasi.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa