Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mh. Albert Chalamila amesikitishwa na matumizi mabaya ya fedha katika ujenzi wa mradi wa bwawa la Lwanyo na kuishauri Wizara ya Maji kuwachukulia hatua za kinidhamu wale wote waliohusika katika ujenzi wa mradi huo.
Mhe. Chalamila ameyasema hayo leo tarehe 25 Semptemba, 2018 wakati akikagua mradi wa maji wa bwawa la Lwanyo katika ziara yake ya kikazi Wilaya ya Mbarali kukagua shughuli za maendeleo na kutatua kero za wananchi.
Amesema kuwa anaishauri wizara kwa sababu mradi huo wakati unajengwa fedha zilikuwa zinapita kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji kuja Ofisi ya Umwagiliaji Kanda ya Mbeya ambao ndio walikuwa wanasimamia ujenzi wa mradi huo.
“Ushauri wangu kwa Mhe Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa ni kuwakamata wale wote waliohusika na ujenzi wa mradi kwa sababu mradi huu umetengenezwa na viongozi waliokosa uadilifu, wala rushwa na wasio na mapenzi mema na nchi yetu” Amesema Mhe. Chalamila.
Amesema kuwa inasikitisha kuona mradi umetumia zaidi ya shilingi bilioni 3.07 bado haujakamilika na ofisi ya umwagiliaji kanda wanaomba fedha nyingine za kwenda kumalizia mradi huo wakati fedha iliyokwisha kutumika na thamani ya mradi haviendani.
Kazi ya ujenzi wa bwawa la Lwanyo ilifanywa na mkandarasi M/s Boimanda Modern Construction Co kwa gharama ya shilingi bilioni 2,951,363,153.70 chini ya usimamizi wa Ofisi ya Mhandisi wa Umwagiliaji Kanda ya Mbeya lakini mpaka kufikia tarehe 15 Disemba, 2013 gharama zilifikia shilingi bilioni 3.077,220,613.21 kutokana na changamoto zilizojitokeza wakati wa ujenzi ikiwemo ya uvujaji wa bwawa kwa sababu ya mapungufu ya uchunguzi wa udongo ardhi na miamba (Geotechnical Investigation Study).
Aidha, Mhe Mkuu wa Mkoa Albert Chalamila amepata fursa ya kutembelea mashamba makubwa ya wawekezaji ya Kapunga Rice Project na Highlands Estate na kufurahishwa na namna makampuni hayo yanavyojitolea kuchangia shughuli za maendeleo katika maeneo yao na kuwaomba kuendelea na hamasa hiyo hasa katika kufanikisha agenda kuu ya Mkoa wa Mbeya ya kujenga Zahanati kila kijiji ifikapo mwaka 2020.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa