Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Albert Chalamila leo tarehe 11 Septemba, 2018 ameendelea na ziara yake Wilaya ya Kyela ambapo ameanza kwa kukagua Ujenzi wa meli tatu zinazogharimu kiasi cha shilingi bilioni 20.1 katika bandari ya Itungi.
Ujenzi huo wa meli unatekelezwa na kampuni ya kitanzania Songoro Marine umejumuisha ujenzi wa meli mbili za mizigo zenye uwezo wa kubeba tani 1000 za mizigo kila moja na meli ya abiria na mizigo yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 200 za mizigo.
Meneja wa Mamlaka ya Bandari Bw. Abed Gallus Abed amemueleza Mhe. Mkuu Wa Mkoa ujenzi wa meli mbili za mizigo za MV Njombe na MV Ruvuma umekamilika mwezi Julai, 2017 na kusajiliwa na Mamlaka ya udhibiti wa shughuli za vyombo vya majini(TASAC) na kuanza safari zake za awali kwenda Mbamba Bay Ruvuma na Nkhata Bay nchini Malawi mwezi Septemba, 2017 kwa MV Njombe na Januari, 2018 MV Ruvuma.
Akizungumza na watumishi wa Mamlaka ya Bandari baada ya kukagua meli hizo Mhe Chalamila amewataka kufanya kazi kwa ushirikiano na kuwa na mkakati wa kuzitangaza meli hizo ili kuvutia wafanyabiashara kutumia meli hizo kwa ajili ya kusafirishia mizigo yao kwenda mikoa ya jirani na nchi ya Malawi.
Mhe Chalamila amemuagiza Meneja wa Mamlaka ya Bandari kutengeneza timu ya wataalamu ambayo itafanya kazi kuwashawishi wafanyabiashara wa Tanzania na Malawi kuweza kupitisha mizigo yao katika bandari hiyo ili kuongeza mapato na idadi ya mizigo katika bandari Kiwira.
Mheshimiwa Chalamila alipata nafasi ya kukagua ujenzi wa barabara ya Kikusya-Ipinda -Matema kiwango cha lami yenye urefu wa km 34.6 ambao una gharama ya shilingi bilioni 56.911 ikiwa ni moja ya mikakati ya Serikali kurahisisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kuboresha mtandao wa barabara wilayani Kyela.
Mhandisi Mshauri wa Wakala wa Barabara Mkoa (TANROADS) Bw. Samuel Joel amesema hadi tarehe 11 Agosti, 2018 maendeleo ya kazi ikiwa ni pamoja na kazi za awali za maandalizi ni asilimia 88.9 na kazi za ujenzi wa barabara pekee zimekamilika kwa asilimia 71.4 na muda uliotumika ni miezi 37 sawa na asilimia 88.1 ya muda wa mkataba yaani miezi 42.
Akizungumza kwenye Mkutano wa hadhara Ipinda Mhe Chalamila amewapongeza Wakala wa Barabara (TANROADS) kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa barabara hiyo na kuwataka kulinda na kusimamia ubora wa barabara ili iweze kudumu kwa muda mrefu.
“Kuna haja sasa ya kuishauri Serikali kuwa miradi ya ujenzi iwe inasimamiwa na wahandisi washauri kutoka serikalini (TANROADS) badala ya kuchukua wataalamu hao kutoka sekta binafsi, kwanza kutapunguza gharama za ujenzi na pili kutasaidia usimamizi wenye ufanisi na kazi na ujenzi zenye ubora” Amesema Mhe Chalamila.
Mhe. Chalamila amewashukuru wananchi wa Ipinda kwa kuamua kubomoa wenyewe nyumba zilizopo kwenye hifadhi ya barabara kupisha ujenzi na kuwataka kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuri kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo.
Aidha, Mhe Chalamila amepata fursa ya kutembelea kituo cha Afya cha Ipinda kilichofanyiwa ukarabati wa Jengo la wagonjwa wa nje na ujenzi wa majengo mapya 11 ikijumuisha jengo la upasuaji, wodi ya wazazi, nyumba ya mtumishi, maabara, jengo la kuhifadhia maiti, kichomea taka, jengo la kufulia, jengo la mionzi, wodi ya watoto, njia za wagonjwa na mfumo wa maji safi na maji taka uliogharimu kiasi cha shilingi 625,899,806 ikiwa ni fedha kutoka serikalini, michango ya wananchi na wadau wa maendeleo
“Nawapongeza Wataalamu wa Halmashauri, Viongozi wa Wilaya na Wananchi kwa usimamizi mzuri wa fedha na kuweza kujenga majengo 11 badala ya 5 kama ilivyoelekezwa na Wizara na kukifanya kituo hiki kuwa kituo cha mfano wa halmashauri nyingine nchini kuja kujifunza hapa”. Amesema Chalamila
Mhe. Chalamila amewashukuru wananchi kwa kuhamasika kuchangia ujenzi wa kituo hicho na kuwaomba kuendelea na hamasa hiyo ya kuchangia shughuli nyingine za kimaendeleo kwenye miradi mingine kwa sababu miradi mingi inahitaji nguvu za wananchi kutekelezwa.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa