Na Nebart Msokwa, MBEYA
MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amewapa siku 14 wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri zote za mkoa huo kuandaa madirisha maalumu kwa ajili ya kuhudumia wazee kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
Alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki wakati wa kikao na wawakilishi wa wazee kutoka katika wilaya zote za mkoa huo kilichofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Mbeya ambapo alisema baada ya siku hizo kumalizika atafanya ziara ya kukagua madirisha hayo kwenye vituo hivyo.
Alisema baada ya siku hizo kuisha hatataka kuona wazee wanapanga foleni kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, kutamkiwa lugha mbaya wala kutakiwa kwenda kununua dawa kwenye maduka ya watu binafsi kwa maelezo kuwa Serikali inapeleka dawa kwa ajili ya kundi hilo kwenye vituo hivyo.
“Haiwezekani wazee wetu wamelitumikia taifa letu kwa uzalendo halafu wawe wanapata shida, sio mzee ana kitambulisho kinachomtaka atibiwe bure halafu anasimama kwenye foleni, kila muda anaambiwa subiri inaweza ikafika muda mzee akaanguka, sasa sihitaji mambo hayo,” alisema Homera.
Aidha alilitaka Jeshi la Polisi kufanya doria za mara kwa mara katika maeneo mbalimbali na kuwachukulia hatua kali vijana wote ambao hawafanyi kazi na badala yake wanacheza michezo isiyoruhusiwa kuchezwa mchana.
Alisema baadhi ya vijana hao ndio wanaofanya matukio ya unyanyasaji dhidi ya wazee ikiwemo kuwaibia, kuwapiga na hata kuwatamkia maneno machafu.
Alisema baadhi ya vijana hao huwa wanavuta bangi na kutumia dawa zingine za kulevya hali ambayo inachochea vitendo vya uharifu kwenye jamii.
Katika hatua nyingine aliwataka wakurugenzi wa halmashauri zote za mkoa huo kuhakikisha zinatenga bajeti kwa ajili ya kushirikiana na Wakala wa Barabara za mijini na vijijini (TARURA) kuboresha barabara huku akilitaka Jiji la Mbeya kutenga Sh. Bilioni moja kila mwaka.
Awali baadhi ya wazee wa Mkoa huo, waliiomba Serikali iwasaidie kuwadhibiti vijana wao kwa maelezo kuwa baadhi ya vijana hao wamekuwa wavivu wa kufanya kazi na badala yake wanashinda wakicheza kamali.
Mmoja wa wazee hao, Halima Mwakitalima kutoka katika Kata ya Ilemi, alisema baadhi ya vijana wao wanavuta bangi na kunywa pombe kali za moshi (gongo) na wakirejea nyumbani wanaanza kuwapiga wazazi wao bila hata sababu.
“Tunaomba mtusaidie maana hatuna amani kabisa, watoto wetu wanakunywa sana pombe na kuvuta mibangi na wakifika nyumbani wanaanza kutupiga na kutudhalilisha wazazi wao,” alisema Halima.
Kwa upande wake mzee Hosea Osasine kutoka katika Wilaya ya Mbarali alimuomba Mkuu wa Mkoa kuwasaidia kutatua migogoro ya ardhi katika Wilaya hiyo kwa maelezo kuwa wazee ndio wanaoathirika zaidi na migogoro hiyo.
Alisema baadhi ya migogoro inayowatesa wananchi wa Mbarali ni ya wakulima na wafugaji, wananchi na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha pamoja na migogoro ya wakulima wadogo na wawekezaji wa mashamba makubwa.
mwisho
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa