Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amesema vitendo vya urasimu na rushwa vinavyofanywa na baadhi ya watendaji Serikalini ndio sumu inayokwamisha kasi ya uwekezaji wa viwanda.
Chalamila aliyasema hayo jana wakati akikagua ujenzi wa kiwanda cha kisasa cha kusindika maziwa kinachojengwa na Kampuni ya Asas Dairies Ltd wilayani Rungwe, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea, kuzindua miradi ya maendeleo na kzungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara.
Alisema wawekezaji wengi wanaojitokeza kutaka kuanzisha viwanda mkoani Mbeya wanakutana na mazingira magumu ya urasimu na kuombwa rushwa na maofisa wa Serikali hali ambayo inawakatisha tama na kuamua kupeleka miradi hiyo maeneo mengine.
“Nimebaini kuwa urasimu na rushwa ndiyo sumu ambayo inakwamisha uanzishwaji wa viwanda mkoani hapa, baadhi ya watendaji mmekuwa na urasimu huku wengine mkithubutu kuomba rushwa ili mkubali kutoa maeneo au vibali vya uanzishwaji wa viwanda,” alisema Chalamila.
Alitoa mfano uwekezaji wa kiwanda cha mbegu ambao unataka kufanywa na kampuni ya Seedco ambao umekwamishwa na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kwa kutokuwa wepesi kuidhinisha eneo la ujenzi wa kiwanda hicho.
Chalamila alisema amebaini kuwa muwekezaji huyo amezungushwa kupewa kibali cha ujenzi wa kiwanda hicho mpaka akakaribia kukata tama na kutaka ahamishe kiwanda hicho kukipeleka mkoa mwingine.
Alisema baada ya kubaini suala hili amekutana na muwekezaji huyo na kumsihi asikate tamaa na kumuahidi kushughulikia changamoto hiyo na kuhakikisha anapewa kibali hicho haraka iwezekanavyo.
“Leo hii ninapozungumza kuna muwekezaji wa kiwanda cha Seedco walikuwa wanapaswa kuondoka kwenda kuanza kuwekeza mahali pengine kwa sababu waliomba ardhi kwa muda mrefu lakini mpaka muda huu tulikuwa bado hatujatoa hiyo ardhi, nimemuagiza Mkurugenzi wa Mbeya vijijini ndani ya siku tano awe amekwishatoa imvoice inayotakiwa kwa ajili ya malipo kidogo ya hiyo ardhi ili tufunge kiwanda kikubwa cha masuala ya mbegu bora kabisa hapa Tanzania,” alisema Chalamila.
Aidha Chalamila aliuagiza uongozi nwa Wilaya ya Rungwe kuanza mkakati wa kupata kiwanda cha kuchakata ndizi ili wilaya hiyo iache kusafirisha ndizi ghafi kwenda Dar es Salaam na badala yake isafirishe bidhaa zitokanazo na zao hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Julius Chalya alisema amepokea maagizo hayo na kudai kuwa wilaya hiyo inayo mazao makuu matano ambayo tayari wamejiwekea mkakati wa kila zao kuwa na kiwanda chake kwa ajili ya usindikaji.
Chalya aliyataja mazao hayo kuwa ni chai, Parachichi, Kahawa, ndizi, maziwa na viazi mviringo.
Alisema mpaka sasa mazao matatu tayari yameshafanikiwa kupata kiwanda kwa ajili ya usindikaji na mengine mawili wanaendelea kutafuta wawekezaji watakaowekeza kwenye maeneo hayo.
“Mpaka sasa tayari tuna viwanda viwili vya kusindika chai, tunacho kiwanda cha maparachini na sasa kiwanda cha maziwa kinajengwa na kimekaribia kukamilika,” alisema Chalya.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Ezekiel Mwankota alisema kuwa Wilaya ya Rungwe kwa sasa inazalisha zaidi ya lita milioni 63 kwa mwaka na kwamba kiwango hicho cha maziwa kinahitaji uwekezaji mkubwa wa viwanda ili maziwa hayo yaweze kusindikwa na kupata bei nzuri.
Alisema mpaka sasa utafiti uliofanyika unaonyesha ni asilimia 11 tu ya maziwa yanayozalishwa wilayani Rungwe ndiyo yanayonunuliwa kwa ajili ya kusindikwa viwandani na mengine yanaishia kununuliwa kwa bei ndogo mitaani kwa ajili ya matumizi ya majumbani.
Alisema uwepo wa kiwanda hicho utasaidia maziwa mengi zaidi kununuliwa viwandani, jambo ambalo pia litaongeza bei ya maziwa kutoka kwa wafugaji, sambamba na kutoa ajira kwa wananchi wa Rungwe.
Awali, Mratibu wa Kampuni ya Asas Dairies Ltd, Lipita Mtimila alimueleza Chalamila kwamba kiwanda hicho kitakamilika June mwakani na kitakuwa na uwezo wa kusindika lita 50,000 kwa muda wa masaa nane
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa