Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Amos Makalla ametoa siku 30 kwa Watendaji wa Kata kuona mabadiliko ya utendaji kazi wao kwa kusimamia na kuhamasisha wananchi kuhusu suala zima la usafi katika Halmashauri za Mbeya Jiji na Mbeya Vijijini.
Akiongea katika kikao kazi cha Watendaji na Viongozi wa Wilaya ya Mbeya katika ukumbi wa Mkapa hivi leo Mhe Makalla amesema kuwa hajaridhishwa na jinsi Watendaji hao wanavyosimamia suala la usafi hasa katika Jiji la Mbeya.
Amesema kuwa Watendaji Kata wengi wana tabia ya kusukumwa katika utendaji kazi wao na matokeo yake kufanya kazi kwa nguvu ya soda na kuacha kufuatilia kabisa suala linavyoendelea.
“Nataka kuona Jiji linakuwa safi ndani ya mwezi mmoja na hicho ndio kipimo chenu kuona kama mnatosha katika nafasi zenu na kwa hili sitakuwa na huruma na mtendaji atakayeshindwa kutimiza wajibu wake” Amesema
Mhe Makalla ameagiza kila mtendaji wa kata kuhakikisha kuwa zoezi la usafi analisimamia kwa kushirikisha kuanzia viongozi ngazi ya Mtaa kwa kuitisha vikako ndani ya siku saba kukubalia namna ya kuweka kata katika hali ya usafi.
Akiongea katika Kikao hicho Mtendaji Kata ya Ruanda Bw. Jumapili Mwasenga amesema kuwa changamoto zipo nyingi ambazo umesababisha taka kukaa kwa muda mrefu bila kupekekwa dampo katika sehemu nyingi
Bw. Mwasenga amesema kuwa ubovu wa magari ya kubebea taka, uhaba wa vitabu vya kukusanyia ada ya taka, ubovu wa barabara ya kuingia dampo ni changamoto ambazo zimesababisha Jiji la Mbeya kuwa katika hali ya uchafu
Aidha Bw. Mwasenga amekiri Watendaji pia kutohamasisha usafi katika maeneo yao na kutosimamia wafanyabiashara wanaofanya biashara katika maeneo yasio rasmi hasa kwenye Hifadhi za barabara na kuzalisha taka nyingi.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya Dk Aman Kilemile amekiri kuwepo kwa tatizo la taka ndani ya Halmashauri yake na kusema kumetokana na tatizo la utendaji ndani ya Idara ya usafi na mazingira.
Dk Kilemile amesma udhaifu uliokuwepo katika idara hiyo kumesababisha kutokuwepo na mawasiliano mazuri ya kiutendaji kati ya Idara na Watendaji Kata na kupelekea tatizo la uchafu kudumu kwa muda mrefu
Amesema kuwa changamoto ya ubovu wa magari ya kubebea taka na ubovu wa barabara zimeshapatiwa ufumbuzi na kwa sasa magari yanandelea na zoezi la kubeba taka.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa