Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mhe. William Ntinika amewataka Madiwani wa Halmashuri za Mbeya kutumia mafunzo elekezi ya Mradi wa PS 3 kama yalivyokusudiwa kwa kuhakikisha wanapata uelewa na maarifa kuhusu uendeshaji wa Serikali za Mitaa, pamoja na wajibu na majukumu yao katika kusimamia uendeshaji wa Mamlaka hizo.
Mhe. Ntinika ameyasema hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya wakati wa ufunguzi wa Semina Elekezi kwa Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti wa Halmashauri Wakurugenzi, Makatibu Tawala wa Wilaya na Wakuu wa Idara kutoka Halmashauri za Rungwe, Mbarali, Kyela, Mbeya Jiji na Mbeya DC chini ya Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS 3) unaofadhiliwa na Watu wa Marekani chini kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo (USAID)
Mhe Ntinika amewashukuru Wafadhili hao kwa kuleta mafunzo hayo ya Madiwani Mkoa wa Mbeya kwa kuwa ni mradi wa kipekee kwa sababu unagusa maeneo ya mifumo ambayo ni maeneo mtambuka kwa sekta zote, kinyume na mazoea ya miradi ambayo inalenga sekta moja.
Mhe. Ntinika amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo waheshimiwa Madiwani katika masuala ya Usimamizi wa Fedha, Uibuaji wa Vyanzo vya Mapato na Usimamizi wa Manunuzi ya Umma katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kusaidia utekelezaji wa kazi za manunuzi ya umma kuwa katika kiwango chenye ubora, usahihi na kuzingatia thamani ya fedha.
Aidha, Mhe. Ntinika amesema kuwa mafunzo haya yatawasaidia na kuwajengea uwezo Madiwani wa kuhoji na kusimamia mambo mbalimbali katika halmashauri kupitia vikao lakini pia yatawawezesha kujifunza mbinu za ushirikishaji na uhamasishaji wa jamii kushiriki katika kuibua na kusimamia miradi ya maendeleo
Naye Dr. Peter Kilima Mkurugenzi wa Mradi wa PS 3 amesema kuwa Mradi upo katika kufanya kazi na Mbeya katika kuimarisha mifumo ya umma na kuhakikisha Wawakilishi wa wananchi wanatimiza wajibu wao kwa kuwashirikisha wananchi ili waende na kasi ya Serikali yao na kazi zitendeke wananchi wapate huduma na kuweza kupata maendeleo.
Mradi huu ulianzishwa na Serikali 2 ya Marekani na Tanzania kukaa pamoja kwa ajili ya kuweza kusaidia katika kuimarisha mifumo ya umma. Mradi huu ni wa Miaka 5 kuanzi 2015 mpaka 2025 unashirikiana na wadau wa Nchi kama Mkapa Foundation, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo cha Serikali za Mitaa Homboro na Tanzania Mentors Association.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa