Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amepiga marufuku magari yote ya matangazo yanayokodiwa kuongoza misafara ya kuchukua miili ya waliofariki kwenye hospitali na majumbani kwa kuwa yanajenga hofu kwa jamii.
Chalamila ametoa agizo hilo leo Jumatatu, Februari 22, 2021 jijini hapa baada ya kufungua mafunzo ya masuala ya afya na kwamba lengo la kutoa katazo hilo ni kutokana na matangazo hayo kutengeneza hofu kwa jamii na kusitisha shughuli za kiuchumi.
"Nimetoa katazo hilo kwani hata mimi nikisikia napata hofu hivyo nimekuwa nikipewa ushauri wa mara kwa mara na wataalam wa afya na kwamba matangazo hayo yanajenga taswira vifo vinavyotangazwa vinahusishwa na ugonjwa wa covid 19.”
"Mbona zamani mtu akipoteza maisha kwa maradhi mbalimbali na kulikuwa hakuna magari ya matangazo sasa kila msiba matangazo barabarani jambo ambalo linaleta hofu kwa wananchi na shughuli za kiuchumi kusimama kwa muda,"amesema.
Amesema kuwa kuanzia tarehe aliyotaja hatahitaji kusikia gari lolote likipita kutangaza na kama familia itahitaji kutangaza wasubiri muda wa ibada kanisani na maeneo ya makaburini wanapokwenda kuwasitiri wapendwa wao.
Kauli hiyo ya Chalamila imeungwa mkono na wakazi jijini hapa wakidai kuwa matangazo hayo yamekuwa yakileta taharuki kubwa kwa jamii na hofu ya vifo hivyo kuhusishwa na corona.
Juma Issa, Mkazi wa Meta amesema kuwa wazo hilo la Serikali ni jema na kwamba urejee mfumo wa miaka ya nyuma mtu akifariki dunia anakwenda kusitiriwa bila msafara mrefu wa matangazo ambayo yanachangia kusitisha shughuli za kiuchumi na hofu kwa wagonjwa wanaougulia majumbani na hospitali zilizopo jirani na miundombinu ya barabara.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa