Na Nebart Msokwa, MBEYA
TATIZO la Jiji la Mbeya kushika mkia kwenye ukusanyaji wa mapato, limeendelea kushikiwa bango ambapo Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amesema amebaini kuwa mapato yanavuja kutokana na baadhi ya watumishi wa jiji hilo kutokuwa waadilifu.
Akizungumza na watumishi wa Jiji hilo jana, Chalamila alisema amebaini kuwa baadhi ya watumishi wanamiliki vibanda vya biashara kwenye masoko mbalimbali lakini wanakwepa kulipa kodi halali za serikali.
Alisema kitendo hicho kinapelekea mapato ya serikali kupotea huku watumishi hao wakijinufaisha kwa kukusanya mapato hayo, hivyo akasisitiza kuwa bila kurekebisha hali hiyo, mapato yataendelea kupotea.
Alisema anaendelea na uchunguzi kwa kutumia vyombo vyake ili kuwabaini watumishi wote wanaomiliki vibanda kwenye masoko hayo na kwamba baada ya hapo hatua zitaanza kuchukuliwa.
“Jiji lina vyanzo vingi vya mapato yakiwemo masoko, lakini ukienda kwenye vibanda vya masoko yetu unakutana na majina ya viongozi, kwenye vibanda hivyo serikali inapata mapato sifuri halafu wenyewe wanapata asilimia nne, hatuwezi kufika,” alisema Chalamila.
Aliwataka viongozi wa Jiji hilo kufanya kazi kwa weledi bila kuingiliana majukumu ili kuinua uchumi ikiwa ni pamoja na kusaidiana kuziba mianya ya mapato kuvuja.
Aliongeza kuwa ajenda ya ukusanyaji wa mapato imeanzishwa na rais Dk. John Magufuli hivyo kila mtu anatakiwa asimamie eneo lake ili kuhakikisha mapato yanakusanywa sawasawa kwa ajili ya kuimarisha huduma za kijamii.
Hata hivyo alisema katika uchunguzi wake ameshawabaini watumishi wanne wa Jiji hilo waliojimilikisha vibanda hivyo vya serikali na kwamba anaendelea na zoezi hilo.
“Kufanya biashara kwenye vibanda vya serikali inaruhusiwa, lakini kutumia vibanda vya serikali kujinufaisha hairuhusiwi, sasa nawahakikishia kuwa nikimaliza uchunguzi nitaanza kuita mmoja mmoja kwa ajili ya mahojiano na hatua zaidi,” alisisitiza Chalamila.
Chalamila alisema uhuni kama huo ulikuwa unafanyika pia kwenye Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kabla tatizo hilo halijathibitiwa na serikali.
Alisema kuna baadhi ya watumishi wamekuwa wakiwaomba fedha watunza hazina wa halmashauri na kwamba wakiwakatalia wanaanza kuwachafua kwa kutumia itikadi za kisiasa za CCM na Chadema.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa