MKUU wa Mkoa wa Mbeya,Amos Makalla ametimiza ahadi yake ya kukabidhi msaada wa Mifuko 100 ya Saruji kwaajili ya kuchangia ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya msingi Iyela iliyopo katika kata ya Iyela jijini hapo.
Kadhalika Makalla amekabidhi msaada wa fedha taslimu shilingi milioni moja kwaajili ya kuchangia ujenzi wa vyoo katika shule ya msingi Ivumwe iliyopo katika kata ya Mwakibete jijini Mbeya.
Akikabidhi msaada huo,mkuu huyo wa mkoa alisisitiza kuwa atazidi kuwaunga mkono wananchi watakaoonesha nia ya kuibua na kuanzisha mradi wa kimaendeleo na si wale wanaobaki kusubiri kila kitu kifanywe na Serikali.
Makalla alisema wakati uliopo ni wa kila mmoja kujiuliza anawezaje kuikwamua jamii inayomzunguka kwa kubuni mradi utakaowezesha kuondokana na changamoto zilizopo kisha kuwashirikisha wadau ikiwemo Serikali.
“Yapo maeneo kila ukienda wanaorodhesha changamoto zinazowakabili,ukiwauliza ninyi mmeanza na lipi katika kutafuta ufumbuzi wanakujibu tunaisubiri Serikali ifanye.Tuna vijiji vingi,kata nyingi hapa mkoani tukisema kila hao wasubiri Serikali ikatatue changamoto tutachelewa lakini wale watakaoanzisha lazima tuwaunge mkono maana maendeleo ni ubia”alisema Makalla.
Mkuu huyo wa mkoa pia aliwasihi wakazi wa maeneo hayo kuachana na wanasiasa uchwara wanaowapotosha wananchi kuwa wadau wanaojitoa kuchangia shughuli za kimaendeleo kwa kutoa misaada wana nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Alisema anachoamini yeye wadau wanaochangia maendeleo wana nia ya dhati ya kuiwezesha jamii kuondokana na changamoto zinazoikabili jamii mkoani hapa na si uchu wa madaraka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa wa Iyela I,Simon Mwakaje alisema ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya msingi Iyela umekuwa wa kusuasua kutokana na wakazi wa eneo hilo kuwa wagumu katika kuchangia licha ya uwepo wa wadau wachache walioonesha nia ya kusaidia.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa