HOTUBA YA MHE. ALBERT CHALAMILA, MKUU WA MKOA WA MBEYA KATIKA UFUNGUZI WA SEMINA YA URAGHIBISHI NA UHAMASISHAJI WA MAGONJWA YALIYOKUWA HAYAPEWI KIPAUMBELE (NEGLECTED TROPICAL DISEASES)
TAREHE 09 OKTOBA, 2018
MBEYA
Ndugu Katibu Tawala wa Mkoa,
Ndugu Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya,
Ndugu Wakurugenzi wa Halmashauri,
Ndugu Mratibu wa Taifa wa Mpango wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele,
Ndugu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,
Ndugu Afisa Elimu wa Mkoa wa Mbeya,
Ndugu Mwakilishi wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali IMA –World Health,
Ndugu Wanasemina,
Waandishi wa Habari,
Ndugu wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana,
Awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetuwezesha kukutana hapa. Aidha, napenda kuwashukuru waandaaji wa shughuli hii kwa kunipa heshima ya kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa semina hii muhimu kwetu sisi wananchi wa mkoa wa Mbeya.
Napenda kuishukuru Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Idara ya Kinga kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele, na Wadau wa IMA World Health kwa kuandaa semina hii muhimu. Aidha napenda kuwakaribisha wale wote waliotoka nje ya Jiji la Mbeya, nasema karibuni sana na mjisikie mpo nyumbani.
Ndugu Washiriki,
Tanzania ni moja kati ya nchi zilizo katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo zinakabiliwa na tatizo la magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele. Magonjwa hayo ni Usubi, Kichocho, Minyoo ya Tumbo, Trakoma (Vikope), Matende na mabusha ambayo baadhi yake yameathiri sehemu kubwa ya jamii yetu katika Mkoa huu wa Mbeya, na kuleta mahangaiko mengi kwa wananchi pamoja na ulemavu, hali ambayo inapunguza uwezo wa wananchi wetu kushiriki katika shughuli mbalimbali za ujenzi wa Taifa. Aidha yamefanya watoto kutoweza kuhudhuria vizuri katika masomo yao shuleni. Magonjwa haya, pamoja na kusababisha usumbufu mkubwa kwa waathirika, pia yanaongeza matumizi ya rasilimali chache tulizonazo katika kuyakabili. Jambo la kutia moyo ni kwamba Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kwa kushirikiana na Wadau wamekuwa wakitoa dawa za kutibu na kukinga magonjwa haya katika Mkoa wetu.
Lengo kuu la Serikali yetu ya awamu ya tano ni kutumia rasilimali chache zilizopo katika kudhibiti magonjwa yanayowasumbua wananchi wake. Hivyo udhibiti wa magonjwa haya chini ya Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele, unatekelezwa kwa pamoja kwa kuunganisha nguvu, hivyo kupunguza gharama za utendaji na kuwafikia Wananchi kwa urahisi.
Ndugu Washiriki,
Juhudi mbalimbali za kuyakabili magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele zimekuwa zikiendelea nchini na mafanikio ya juhudi hizi yameanza kuonekana katika kuyatokomeza. Kwa Mkoa wetu wa Mbeya tulikuwa tunakabiliana na magonjwa yote matano yaani Minyoo ya tumbo, Kichocho, Matende na mabusha katika wlaya zote, Trakoma au Vikope, katika wilaya za Kyela, Chunya na Mbarali, ugonjwa wa Usubi katika wilaya za Rungwe, Kyela na Busokelo. Taarifa nilizozipata ni kwamba Mkoa wetu umeweza kupunguza kiwango cha maambukizi kwa magonjwa ya Trakoma, Matende na mabusha, na hivyo kupelekea kusimamisha zoezi la umezeshaji wa dawa katika kudhibiti magonjwa hayo katika ngazi ya Jamii. Nawapongeza sana wote waliofanikisha hili na hasa wananchi ambao waliitikia wito wa kumeza dawa. Kwa ugonjwa wa Usubi Mkoa wetu unafanya vizuri katika juhudi za kutomeza ugonjwa huo, na kwa taarifa nilizonazo ni kwamba tunasubiri maelekezo kutoka Shirika la Afya Duniani ili nao tuweze kusitisha unywesheshaji wa dawa. Hivyo hamasa iendelee kuwahamasisha wananchi kushiriki katika mazoezi yaliyo mbele yetu ya umezeshaji wa dawa katika ngazi ya jamii kwa ajili ya kutokomeza kabisa ugonjwa huu wa Usubi. Aidha kwa magonjwa ya Kichocho na Minyoo ya tumbo bado ni tatizo kwa jamii yetu hivyo nitoe rai kwa Viongozi wote wa Halmashauri zote za Mkoa wa Mbeya kuwa na jitihadi za ziada kuelimsha jamii zetu washiriki kikamilifu kumeza dawa za kingatiba mara mazoezi hayo yanapotokea.
Ndugu Washiriki,
Nimefahamishwa kwamba zoezi la utoaji wa Kingatiba ya dawa ya Mectizan kwa ajili ya kutokomeza ugonjwa wa Usubi kwa wananchi wa Wilaya za Rungwe, Kyela na Busokelo hivi sasa linaendelea katika maeneo yenu. Pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali na Wadau kutuletea dawa hadi katika ngazi ya chini, naomba nitoe rai kwa Viongozi wote wa Wilaya hizi kusimamia kikamilifu zoezi hilo na kuhakikisha kwamba idadi kubwa ya wananchi wanajitokeza kupewa Kingatiba hiyo ili tuweze kufikia malengo yanayohitajika na kuweza kuutokomeza ugonjwa katika Mkoa wetu wa Mbeya. Napenda kusisitiza kuwa pamoja na kwamba tunapata uhisani wa fedha za kuendesha zoezi hilo kutoka kwa Wadau, tukumbuke kwamba wenye dhamana ya Afya ya wananchi wetu ni sisi wenyewe Viongozi wa Mkoa na Wilaya. Hivyo basi, kila Kiongozi wa Halmashauri ahakikishe zinatengwa fedha kwa ajili ya kuendeshea zoezi hilo tuweze kufikia lengo la Shirika la Afya Duniani la kutokemeza ugonjwa huu.
Ndugu Washiriki,
Leo tuna timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, wamekuja wakiwa wamejiandaa kikamilifu kutupatia hamasa na elimu juu ya mpango huu na uendeshaji wake. Naomba washiriki wote tuwe makini na wasikivu, ili tuweze kutoka na hamasa na elimu ya kutosha juu ya magonjwa haya na kile tutakacho kipata hapa tuwapelekee wenzetu katika maeneo yetu hatimaye wananchi wetu waweze kunufaika na Mpango huu, na kuondokana na matatizo haya na kuweza kuchangia kikamilifu katika pato la Taifa. Kwa hiyo, ni matumaini yangu ya kwamba elimu watakayotupatia leo itakuwa ni faraja kubwa kwetu sisi Viongozi na tuweze kuifikisha kwa wananchi wote wa Halmashauri zetu.
Mwisho,
Ninakutakieni nyote usikivu na ufuatiliaji mwema katika yote yatakayoongelewa kwenye semina hii. Kwa haya machache, napenda kutangaza rasmi kuwa, semina yetu ya uraghibishi na uhamasishaji kuhusu magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele imefunguliwa rasmi.
Asanteni kwa kunisikiliza.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa