Serikali imetenga kiasi cha fedha shilingi bilioni105 za kitanzania kwaajili ya ujenzi wa Hospitali 67 za Wilaya katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2018/19 ili kuiwezesha kuwa na jumla ya Hospitali 137 za Wilaya ambazo zitasaidia kuimarisha hali ya utoaji wa huduma za afya nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo aliyasema hayo akiwa ziarani mkoani Singida katika Halmashauri ya Manyoni alipofika kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha Afya Kintinku katika Halmashauri hiyo ambacho kilikuwa miongoni mwa vituo vya mwanzo vilivyo pokea shilingi milioni 500 za kitanzania katika awamu ya kwanza ya ukarabati wa vituo vya afya 210 kote nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo mara baada yakujionea miundombinu mbali mbali iliyo jengwa na mingine kukarabatiwa ikiwepo Jengo la Upasuaji, Wodi ya Mama na Mtoto, Maabara, Jengo la kuhifadhia Maiti pamoja na Nyumba ya Mtumishi, Waziri Jafo alisema mara baada yakufanya kazi kubwa katika vituo vya afya nguvu kubwa sasa inahamishiwa katika Hospitali za Wilaya.
“Toka tupate uhuru nchi yetu ilikuwa na Hospitali 70 tu za wilaya zinazo milikiwa na serikali ikilinganishwa na idadi ya Halmashauri tulizo nazo sasa 185 utaona kabisa bado tunao uhitaji, hivyo Mhe. Rais anakwenda kuweka historia kwa kujenga Hospitali mpya 67 za Wilaya katika kipindi cha muda mfupi” alisema Waziri Jafo na kuongeza kuwa hayo ni mafanikio makubwa katika historia ya nchi yetu.
Mbali na kuelezea mipango ya Serikali katika kuboresha huduma mbali mbali ikiwepo suala la afya nchini, Waziri huyo vilevile aliwahimiza wananchi kujiunga na mfuko wa Afya ya jamii iliyo boreshwa (Improved Community Health Fund ICHF) ili waweze kupata matibabu kwa wepesi lakini pia kuiwezesha serikali kuimarisha huduma za afya kwakuwezesha upatikanaji wa madawa pamoja vifaa tiba vingine.
“Ndugu zangu hapa kijijini ukiuza kuku wako Majogoo wawili watakuwezesha wewe na familia yako kupata matibu ndani ya mwaka mzima kwa kiasi cha Tsh.30,000 tu hivyo niwaombe mlione hilo na mchukue hatua” alinukuliwa Waziri Jafo.
Katika hatua nyingine Waziri pia aliwataka wanachi wa Vijiji vinavyozunguka na kupatiwa huduma katika kituo cha Afya Kintinku na sehemu zingene nchini kuwa walinzi wa miundombinu ya afya katika vituo hivyo ili viweze kutoa huduma za afya kwa muda mrefu.
Halmashauri ya Manyoni ni miongoni mwa Halmashauri zilizopatiwa fedha za ukarabati wa vituo vya afya vya Kintinku na Nkonko, ambapo katika awamu ya kwanza walipatiwa shilingi milioni 500 za kitanznia zilizo fanya ukarabati katika kituo cha afya Kintinku na katika awamu ya tatu Halmashauri hiyo imepelekewa kiasi cha shilingi milioni 400 za kitanzania kwa ajili ya ukarabati wa kituo cha Afya Nkonko, ukarabati unaotazamiwa kuchukua muda wa wiki 20 hadi kukamilika kwake.
Anaandika Atley Kuni- OR TAMISEMI
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa