Na Grace Mwakalinga, Karonga Malawi
MSAADA wa Tani 200 za Mahindi na Tani 15 za Dawa, Magodoro na Vyandarua ambao umetolewa na Rais Dk. John Magufuli kwa watu walioathirika na mafuriko nchini Malawi umewasili na kukabidhiwa kwa Serikali ya Malawi kwa ajili ya kuwafikishia waathirika wa maafa hayo.
Malori manane ambayo yalibeba Shehena ya Tani 200 za Mahindi na moja lililosheheni dawa, Magodoro na Vyandarua yaliwasili wilayani Karonga yakitokea Tanzania yakitumwa na Rais Dk. John Magufuli .
Msaada huo ulikabidhiwa juzi nchini Malawi na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya , Wiliam Ntinika ambaye aliiwakilisha Serikali ya Tanzania.
‘’Tunakabidhi msaada huu ambao umetolewa na Rais Magufuli nchini kwa Rais wa Malawi Mutharika tani 200 za mahindi, dawa, magodoro na vyandarua msaada huu tunaihakikishia serikali ya Tanzania msaada umeufika hapa Malawi ukiwa salama’’, alisema Ntinika.
Hata hivyo msafara huo wa malori kuelekea Wilaya ya Karonga, nchini Malawi uliongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Claudia Kitta ambaye alisema kuwa msaada huo ni alama ya upendo na undugu uliopo baina ya Tanzania na Malawi
Alisema Serikali ya Tanzania ilitoa msaada huo kutokana na kuwepo kwa mahusiano mazuri baina ya wananchi wa Malawi na Tanzania na kusisitiza kuendelea kushirikiana kwa nyakati zote.
Akipokea Msaada huo kwa Niaba ya Serikali ya Malawi, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kalonga, Raphael Mkisi aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa msaada huo huku akisema kuwa Wilaya 13 kutoka mikoa Saba ya Malawi zimeathirika na mafuriko hayo ambayo yamesababisha zaidi ya watu 60 kupoteza maisha.
Mkisi alisema msaada huo mkubwa utasaidia kuzipa pengo la uhitaji ambalo limetokea kwa sababu ya mafurikio hayo ambayo mbali na kusababisha vifo pia yameharibu miundombinu ya barabara na majengo nchini humo.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa