SHILINGI Bilioni 3.7 zimetolewa na Serikali kwa ajili ya kuboresha miradi ya ujenzi barabara mbalimbali itakayotekelezwa Jijini Mbeya kwa kiwango cha lami na kusimamiwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA)
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe Amos Makalla alibainisha hayo kwenye uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa kipande cha barabara cha kutoka Isyesye hadi Relini jijini Mbeya chenye urefu wa kilomita 2.3.
Mhe Makalla amesema ujenzi wa kipande hicho cha barabara kitakachonufaisha kata za Isyesye na Itezi utagharimu Shilingi milioni 881.
Amesema kuwa Serikali imetenga fedha hizo kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami jijini hapa na kurahisisha shughuli za usafirishaji kupitia miundombinu rafiki.
Aliwapongeza wakazi wa kata ya Isyesye waishio jirani na barabara kwa ushirikiano walioonesha kwa Serikali kwa kukubali kwa hiyari kubomoa bila fidia sehemu ya nyumba zilizokuwa ndani ya eneo linalopaswa kufikiwa na barabara.
“Serikali inapenda watu walio na ushirikiano. Na ndiyo sababu sisi tumejipanga popote walipo wananchi wanaoonyesha ushirikiano tutapeleka miradi. Hatutaki watu wanaokaa kuhamasisha itikadi za vyama badala ya Kuhamasisha maendeleo katika maeneo yao” alisisitza Makalla.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Isyesye, Bw Ibrahim Mwampwani alisema barabara ya lami ilikuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu na wakazi wa kata za Isyesye na Itezi kutokana na adha waliyokuwa wakiipata hususani nyakati za mvua nyingi.
Alisema kujengwa kwa barabara hiyo kutakuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo situ kwa wakazi wa kata hizo mbili bali na maeneo mengine kwakuwa watu wengi wataitumia badala ya kulazimika kupita barabara kuu pekee.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa