SERIKALI kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Mbeya, imeamua kuendelea na ujenzi wa barabara ya Kikusya – Ipinda – Matema katika Wilaya ya Kyela, licha ya baadhi ya wakazi wa Mji wa Ipinda kufungua kesi mahakamani kupinga nyumba zao kubomolewa.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, msimamizi wa mradi huo kutoka katika Kitengo cha ushauri wa kihandisi TANROADS (TECU), Mhandisi Samwel Mwambungu, alisema kitendo cha wananchi hao kufungua kesi kimesababisha mradi kuchelewa kukamilika.
Mhandisi Mwambungu amesema kutokana na umuhimu wa barabara hiyo kwa wananchi wa maeneo hayo, wameamua kuendelea na ujenzi kutokana na eneo lililopo huku nyumba za wananchi hao zikiachwa kama zilivyo.
Mhandisi Mwambungu, amesema barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 34.6 inajengwa kwa kiwango cha lami na Mkandarasi China New Era International Engineering Corporation kwa gharama ya shilingi milioni 56.9 na kwamba mradi unatekelezwa na serikali kwa asilimia 100.
“Mradi ulianza kutekelezwa julai 31, 2015 na ulitakiwa kukamilika ndani ya miezi 24, lakini mpaka sasa haujakamilika kutokana na baadhi ya changamoto ikiwemo baadhi ya wananchi kufungua kesi mahakamani wakipinga kupisha upanuzi,” alisema Mhandisi Mwambungu.
“Tumeamua tuendelee na ujenzi lakini kwenye eneo ambalo hawa wananchi wamegoma, tunajenga kulingana na eneo lililopo bila kugusa nyumba zao,”
Vilevile alisema Mkandarasi wakati mwingine huwa anakwama kutokana na Serikali kumcheleweshea malipo yake, kwa maelezo kuwa mpaka sasa amelipwa shilingi bilioni 7.2 kati ya bilioni 26 anazodai kulingana na kazi aliyoifanya.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Amos Makalla, ameshangazwa na kitendo cha wananchi hao kuishtaki Serikali kwa madai kuwa barabara hiyo ni faida yao wenyewe na hivyo walichokifanya wanajiumiza wenyewe.
Mhe. Makalla amesema barabara hiyo ikikamilika itafungua fursa nyingi kwao ikiwemo kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mizigo kutoka katika maeneo yao na kupeleka maeneo ya masoko ikiwemo kupeleka Kyela mjini na Mbeya.
Aidha Mhe Makalla amesema barabara hiyo itafungua fursa kwenye sekta ya utalii kwa madai kuwa fukwe za Ziwa Nyasa katika eneo la Matema ni kivutio kikubwa cha watalii hivyo wananchi hao watanufaika kwa kuwaongoza watalii na kuwauzia bidhaa mbalimbali wanazozalisha.
“Mtunze kumbukumbu vizuri kwa kile mlichokifanya hapa, watoto wenu na wajukuu watakapowauliza kwanini barabara nyembamba hapa, mkawambie tuliipeleka serikali mahakamani ndio maana ikaamua kujenga hivyo,” alisema Makalla.
Hata hivyo Makalla amesema anakusudia kwenda kuonana na Waziri wa Ujenzi Prof. Makame Mbarawa ili kushawishi Mkandarasi wa barabara hiyo aendelee kulipwa fedha za mradi huo pamoja na kumuomba aidhinishe kipande kinachobakia kuanzia Tenende kwenda Kyela kiunganishwe kwenye Mkataba.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Claudia Kitta, aliishukuru Serikali kwa kuamua kujenga barabara hiyo akidai kuwa itakuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo.
Alisema ni nadra barabara ya kiwango kama inayojengwa katika eneo hilo kutoka mjini kwenda kijijini, hivyo akawataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Mkandarasi.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa