Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe Albert Chalamila ametaka Meneja wa Wakala ya Barabara Mkoa kuhakikisha inafuatilia kwa karibu malipo ya kiasi cha shillingi Milioni 571.99 ya mkandarasi anayejenga barabara ya Igawa- Rujewa –Ubaruku ili asifunge barabara hiyo.
Mhe. Chalamila ameyasema hayo leo alipokuwa akikagua barabara hiyo yenye urefu wa km 6.6 na kusema TANROADS wahakikishe wanansimamia malipo ya mkandarasi huyo ili aweze kukamilisha barabara hiyo kwa wakati.
Chalamila amesema kuwa utovu wa nidhamu wa kujenga barabara chini ya kiwango unaweza kuanza kama mkandarasi ataendelea kucheleweshewa fedha zake na kuisababishia serikali hasara.
Mhe Chalamila amesema ofisi yake ipo tayari kushirikiana na wakala wa barabara kuiomba Wizara ya ujenzi kuwahisha fedha hizo kama wataona kuna uhitaji wa ofisi ya mkoa kuingilia kati suala hilo.
Akisoma taarifa ya Mradi huo Mhandisi Fredy Kipamila amesema kuwa barabara ya Igawa-Rujwa-Ubaruku inajengwa kwa kiwango cha lami ili kurahisisha usafiri na kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi wilayani Mbarali.
Mhandisi Kipamila amesema mradi huo ulitengewa jumla ya sh. Bilioni 6.239 kazi inayofanywa na kampuni ya Summer Communications kwa kushirikiana na kampuni ya Mtwivila Traders zote za Tanzania kwa mkataba wa miezi 12.
Mhandisi amesema hadi agosti 2018, ni asilimi 63 imekamilika ambapo mkandarasi amemaliza kazi ya ujenzi wa tuta la barabara na mhimili wa kwanza wa barabara kwa kuchanganya kifusi na sementi (sub-base) yenye unene wa sentimita 15.
Naye Mhandisi wa Mradi Bw. Herifrey Mgeni ameomba serikali kuwahisha maombi yao ya fedha ili waweze kumaliza barabara hiyo kwa wakati kama ilivyopangwa awali.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa