Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mbeya imeagizwa kuanza kukagua risiti za manunuzi ya saruji kwa mawakala wa kiwanda cha saruji Mbeya katika kipindi cha wiki mbili zilizopita ili kubaini chanzo cha mfumuko wa bei ya bidhaa hiyo.
Agizo hilo limetolewa na mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila leo Ijumaa Novemba 13, 2020 baada ya kufanya ziara ya katika kiwanda cha Saruji Songwe hicho kilichopo Wilaya ya Mbeya Vijijini.
Chalamila amefika kiwandani hapo na kushuhudia wafanyakazi wakiendelea na uzalishaji na magari yakiwa kwenye foleni za kupakia saruji kwa ajili ya kusafirisha kwenda mikoani mbalimbali.
Akizungumza na uongozi wa kiwanda hicho, Chalamila amesema lengo la ziara yake ni kutaka kujua sababu ya mfumuko wa bei kama umeanzia kiwandani au la.
"Nimefika hapa ni kutokana na hali ilivyo mitaani kwa watumiaji wa saruji kwani gharama imepanda kwa kasi sana. Nikiwa kama kiongozi wa Mkoa nimelazimika kufika kujua hali halisi,” amesema.
Amesema tayari amejiridhisha kuwa chanzo sio wawekezaji bali ni mawakala, “sasa ni vyema TRA kufuatilia kuwabaini ili hatua za kisheria zianze kuchukuliwa. Nashangaa mitaani kwenye maduka saruji inauzwa kati ya Sh22,000 wakati hapa kiwandani pamoja na VAT inauzwa Sh14,500 jambo ambalo linawanyonya wananchi wa kipato cha chini.”
Mkuu huyo wa Mkoa amesema ameandika barua wizara ya viwanda kuomba kifanyike kikao cha pamoja kati ya mawakala wa usafirishaji na wawekezaji wa viwanda vya saruji.
Meneja uzalishaji wa kiwanda hicho, Godwsten Mende amesema kiwanda hakijaongeza bei ya saruji sokoni, ongezeko limetokana na uhitaji mkubwa wa watumiaji na awali baada ya kupata taarifa za baadhi ya viwanda kusitisha uzalishaji wao waliongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya wakazi wa Mbeya.
Amebainisha kuwa changamoto kubwa ni usafirishaji wa saruji kutoka kiwandani kwenda kwa mawakala mawakala ambao wanafidia gharama za usafirishaji kwa kupandisha bei ya bidhaa hiyo.
Bw. Gembe ameiomba Serikali kuboresha usafiri wa reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) kwa kuongeza idadi ya vichwa vya treni za mizigo ili iwe fursa kwa kiwanda hicho kuwafikia wateja mikoani.
Mkazi wa Uhindini Mbeya, James Joram amekifananisha kitendo cha wafanyabiashara kupandisha bei ya saruji na uhujumu uchumi na kuitaka Serikali kusaka mwarobaini ili kuwawajibisha.
Fundi ujenzi Oscar Mwaifwani amesema awali walikuwa wakinunua mfuko wa saruji kwa Sh16,000 mpaka Sh17,000 lakini kwa kipindi cha wiki mbili imepanda mpaka kufikia Sh22,000 mpaka Sh24,000 kwa mfuko.
"Hii ni changamoto kwetu mafundi na tunaoshika tenda kubwa za miradi ya ujenzi kwani tayari tulikuwa tumepiga hesabu za manunuzi ya vifaa na inapotokea bei imepaa ni shida,” amesema.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa