Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Mbeya imependekeza kwa pamoja kubadilishwa kwa jina la Uwanja wa Ndege wa Songwe kuitwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mbeya (MIA)
Mapendekezo hayo yalitolewa na wajumbe wa Kamati hiyo katika kikao kilichofanyika jana Ukumbi wa Mkapa na kusema kuwa kumekuwa na mkanganyiko wa mahali ambapo uwanja huo upo.
Akiongea katika Kikao hicho Mwenyekiti wa kamati Mhe. Amos Makalla alisema kuwa kuwepo kwa Mkoa na Wilaya mpya iliyobeba jina la Songwe kumeleta changamoto ya utambuzi sahihi wa maeneo na miundombinu inayotumia jina hilo.
Mhe. Makalla alisema changamoto hiyo imeleta mkanganyiko mkubwa hususani kwa wageni mbalimbali wakiwemo watalii, wasafiri, wawekezaji na hata Watendaji wa Serikali kujua eneo halisi la uwanja huo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mbeya Bw Mwalingo Kisemba alisema kuwa lengo la kubadili jina ni kufanikisha kwa urahisi mikakati ya mkoa ya uwekezaji, biashara na utalii ili kuwarahisishia wawekezaji namna ya kuutambua mkoa na miundombinu yake.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chunya Bw. Bosco Mwanginde alisema kuwa mkanganyiko huo wa jina la uwanja umepelekea wawekezaji kudhani kuwa miundombinu hiyo ipo Mkoa wa Songwe badala ya Mkoa wa Mbeya na kuupunguzia mkoa sifa ya kuwepo kwa miundombinu rafiki kwa ajili ya uwekezaji.
Ujenzi wa uwanja wa Songwe ulizinduliwa rasmi mwaka 2001 na kuanza kutumika mwaka 2012. Jina la Uwanja wa Songwe lilitokana eneo ambalo uwanja huo upo na uwepo wa mto Songwe eneo hilo.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa