Naibu Waziri Ofisi ya Rais-Tamisemi, Mwita Waitara amewataka wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi kuhakikisha ubora wa mazao na ufugaji unaonekana kwenye mabanda ya maonyesho nanenane unafika mpaka kwenye ngazi ya vijiji nchini.
Waitara alitoa agizo hilo alipohutubia washiriki wa maonyesho ya wakulima maarufu kwa jina la Nanenane Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kwenye Uwanja wa John Mwakangale wakati alipozindua rasmi leo (Jumatano).
Awali kiongozi huyo alikata utepe kwenye geti kuu la kuingia viwanja hivyo na pia alitembelea mabanda mbalimbali ambapo alijionea bidhaa zinazoonyeshwa ikiwamo mifugo hai.
“Nimetembelea mabanda mengi yakiwa na mifugo naa mazao bora huku mengine yamesindikwa jambo ambalo sasa naagiza sura ya mabanda haya ifike hadi vijijini. Huko vijiji kuwe na mbegu bora, mbolea na mazao yalimwe kwa kufuata kanuni bora za kilimo kama inavyoonekana kwenye mabanda hapa’’ alisema.
Alisema vijana wasaidiwe ili walime kisasa na wapate tani saba hadi 10 za mahindi kwenye ekari moja badala ya tani 2 huku wafugaji wa ngombe wakipata lita 22 kwa siku badala ya lita sita za maziwa.
Waitara aliwataka viongozi wote wa mikoa, wilaya, ,halmashauri na vyuo vya kilimo kuwasaidia vijana na wanawake katika kuboresha kilimo, ufugaji na uvuvi ili kufika malengo ya Serikali kuhusu uchumi wa viwanda.
“Hakikisheni pembejeo zinapatikana kwa wakati na kwa gharama nafuu hususan mbegu bora na mbolea ‘’ alisema huku akiwataka pia wakurugenzi wa halmashauri kuwasimamia vizuri maofisa ushirika ili wasiwe chanzo cha migogoro kwenye vyama vya ushirika.
Kuhusu suala la uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa , Waitara aliwataka wakazi wa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, kuwachagua viongozi wenye nia ya kushirikiana na Serikali ya awamu ya tano katika kuleta maendeleo.
Alisema Rais John Magufuli ameonyesha njia kwa Watanzania kujiletea maendeleo jambo ambalo watu wanaotaka uongozi wa Serikali za Mitaa lazima walitambuena kuwa tayari kutekeleza.
Awali , Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Albert Chalamila akizungumza kwenye hafla hiyo alisema viongozi wa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ambayo ni Ruvuma, Njombe, Iringa, Songwe, Mbeya, Katavi na Rukwa wamejipanga vema kuongeza kasi ya kusimamia kazi za kilimo, ufugaji na uvuvi kutekeleza vema masuala ya uchumi wa viwanda.
Chalamila alisema maonyesho hayo yanazidi kuwaunganisha viongozi wote na wananchi katika kutekeleza vema mkakati wa kutokomeza umasikini nchini.
Maonyesho hayo yanazidi kushika kasi na yanatarajiwa kufungwa na Waziri Mkuu Mstaafu wa Serikali ya awamu ya nne Mizengo Pinda.
Imeandaliwa na Kitengo cha Habari kamati ya maandalizi ya Maonyesho ya nanenane kanda ya Nyanda za Juu Kusini
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa