Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe Chalamila amewataka wakuu wa idara katika halmashauri kutambua na kuelewa mipaka ya majukumu ya kila mmoja, kuibua mapendekezo yanayoweza kuibua miradi mbalimbali ya maendeleo na uwekezaji wa viwanda kwa kutumia rasilimali zetu na kuacha kuilalamikia serikali.
Mh. Albert Chalamila leo Septemba 12, 2018 ameendelea na ziara yake Wilaya ya Rungwe ambapo alipata nafasi ya kuongea na watumishi wa umma na kuwataka wakuu wa idara kuwa wabunifu ili kuleta tija kwa serikali katika maeneo yao.
“ na mimi nimesema kuwa mkuu wa idara au mtumishi mwingine yeyote asiye mkuu wa idara atakayeandika andiko lake vizuri, mimi kila andiko nitampa shilingi 1,000,000 andiko kuhusu maboresho ya shule, maji, zahanati au viwanda” Amesema Chalamila.
Mhe Chalamila amesema Wilaya ya Rungwe inaongoza kwa kuwa wazalishaji wakubwa wa mazao ya kilimo lakini mpaka leo hakuna mpango mkakati wowote wa uwekezaji wa viwanda na kuwataka wataalamu kuacha kubishana kuhusu masuala ya wawekezaji kwa sababu wanalipotezea muelekeo taifa.
“Nimeambiwa hapa kuna Heifer International na ASAS Group lakini hakuna kinachoendelea, Kuna matatizo Rungwe na kama tutaendelea kubishana sisi wataalamu kwa maslahi yetu wenyewe tunalipotezea taifa muelekeo. Ni kitendo cha fedheha na aibu unapokuta mwekezaji analia kwamba ameombwa rushwa ndipo aje awekeze” Amesema Chalamila.
Amefafanua kuwa inashangaza kuona mikoa mikubwa inayozalisha chakula kwa wingi haijawahi kuwa na mpango wa kuwa na kiwanda kikubwa cha mbolea au viwanda vya kuongeza thamani mazao na kufanya mpaka leo wakulima kuendelea kusafirisha ndizi na viazi kwenye magari badala ya kufanya ‘package’ na kusafirisha kwa kutumia usafiri wa ndege na watu wakala chakula kilikikiwa katika hali ya upya.
Aidha, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa Albert Chalamila amepata fursa ya kutembelea na kukagua ujenzi na ukarabati wa chuo cha Ualimu cha Mpuguso unaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 9.6 ambao unajengwa na Wakandarasi wawili wa Lukolo Company Limited na Salem Construction Limited.
Mkataba wa Lukolo Company Limited unagharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.8 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, maktaba, maabara na ukarabati wa mabweni mawili na vyoo na Salem Construction Limited ambaye ana mradi wa ujenzi wa mabweni mawili, nyumba nne za watumishi, ukarabati wa nyumba 4, kujenga tanki la kuhifadhia maji na kujenga nyumba ya huhifadhia maji kwa mkataba wa shilingi billion 5.7.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa