Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe Albert Chalamila amewataka watumishi wa umma halmashuri ya Kyela kuelewa misingi ya utumishi wa umma na kuacha mihemko ya kisiasa na kushindwa kuwahudumia wananchi.
Mhe.Mkuu wa Mkoa ameyasema hayo leo alipokuwa akiongea na watumishi mbalimbali wa halmashauri na taasisi za umma kwenye ziara ya kujitambulisha na kusema kuwa hakuna demokrasia isiyo dhibitiwa na sheria na kanuni
Mhe Chalamila amewataka watumishi wa umma kuwa waadilifu na kutumia vizuri mamlaka waliopewa na kutokuwa chanzo cha kuongeza malalamiko ya wananchi kwa Serikali bali wametakiwa kutoa huduma bora kwa kuangalia sera na agenda ya nchi kwa sasa.
Amewataka Maafisa mipango na biashara kujitafakari wanaisaidia vipi halmashauri yao na kuagiza wataalamu hao kuwa wabunifu kwa kuandika maandiko ya kutengeneza vitega uchumi vinavyoweza kusaidia na kuiongezea halmashauri mapato ya ndani katika sekta za afya, elimu, viwanda na utalii.
Katibu Tawala wa Mkoa Bibi Mariam Mtunguja amewataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa ushirikiano na kusema kuwa wataalamu wa kiutendaji ndio wasaidizi wakuu wa Mkuu wa Mkoa katika kutekeleza majukumu ya maendeleo katika mkoa na hivyo ni muhimu kuwa na ushirikiano wa karibu katika utendaji kazi.
Aidha, Mhe Mkuu wa Mkoa amepata fursa ya kutembelea kituo cha forodha katika Mamlaka ya Mji Mdogo Kasumulu na kukitaka kituo hicho kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato na kusema jambo hili linawezekana kama taasisi zote zitafanya kazi kwa pamoja ili kubadilishana ujuzi katika maeneo yao.
Ameitaka mamlaka ya forodha kukaribisha mawazo tofauti ya jinsi ya kutanua uwezo wa ukusanyaji wa mapato kwa kushirikisha mawazo mapya kutoka kwenye mamlaka nyingine ikiwa pamoja na wananchi wa eneo husika.
Mhe Chalamila ameitaka mamlaka hiyo pia kusimamia ulinzi na usalama wa mpaka kwa kuimarisha ulinzi na watu wajue kuwa mpaka unalindwa kwani eneo hilo ni rahisi kupitika kwa wahamiaji haramu na magengo.
“kuna baadhi ya watumishi sio waadilifu katika kusimamia ulinzi wa mipaka lakini na walio waadilifu wanaitwa “wanoko”. Ni bora kuitwa “mnoko” kwa kusimamia sheria na kanuni za nchi kuliko kupendwa kwa kuvunja sheria na taratibu za Serikali” alifafanua Mkuu wa Mkoa.
Kamanda wa Polisi Mkoa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi Ulrich Matei amewataka watumishi wa mamlaka hiyo kufanya kazi kwa kushirikiana kwa sababu mpaka huo umekuwa ukitumika sana kwa njia za panya kupitishia magendo, dawa za kulevya pamoja na wahamiaji haramu.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi Matei amewataka pia kuangalia ulinzi na usalama wa bidhaa zinazotoka na kuingia katika mpaka huo ili kujua madhara yake na kuhakikisha wanafunga njia zote za panya zinazotumiwa na wafanyabiashara kupitisha magendo hayo.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa