Waziri Mkuu Mstaafu wa Serikali ya awamu ya nne, Mizengo Pinda amewashtua viongozi wa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na viongozi wengine wa wilaya alipowaambia mikoa yao ni miongoni mwa mikoa 10 inayoongoza kwa utapiamlo wa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano nchini.
Pinda ametoa kauli hiyo leo Agosti 8, wakati akifunga maonyesho ya wakulima, wafugaji na wavuvi wa mikoa hiyo yaliyofanyikakwenye uwanja wa John Mwakangale jijini Mbeya.
Amesema kitaifa asilimia 33 ya watoto 100 wanautapiamlo, lakini mkoa wa Ruvuma una asilimia 40 yawatoto 100 wenye utapiamlo , wakati mkoa wa Iringa una asilimia 47.1 , Mbeya asilimia 33.8, na Mkoa wa Rukwa ni asilimia 47.9.
Mikoa mingine ni Njombe ambao una asilimia 53,mkoa wa Katavi una asilimia 33.7 na Mkoa wa Songwe una asilimia 43.3 idadi ambayo alisema ni kubwa na inatia aibu kwa mikoa inayotajwa kuongoza kuzalisha chakula.
Mwaka 2018 mikoa hiyo yenye watu zaidi ya watu milioni nane ilizalisha kwa asilimia 124 ya malengo na hivyo kuwa na ziada yatani milioni 3.2 ya chakula .
Pinda ambaye anajulikana kwa jina la mtoto wa mkulima amesema tatizo hilo ni la hovyo na kuwataka wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi kuanzisha mkakati maalumu wa kupambana na utapiamlo kwa watoto haona wajawazito ili kuondoka na aibu.
Amesema jambo hilo limemfanya yeye kwa kushirikiana na wadau kuanzisha taasisi itakayofanya kazi ya kupambana na utapiamlo nchini hususan mikoa inayoongoza kwa tatizo hilo.
Ameitaka mikoa yote kushirikiana na na vyuo mbalimbali kutatua changamoto za jamii hususan suala la kutoa elimu kuhusu lishe bora.
Akizungumzia ujasiriamali wake kwa ufugaji wa samaki alisema yeye anamiliki mabwawa tisa Dodoma yaliyochimbwa kwa gharama ya sh 3.5 milioni na kuweka samaki ambao akivuna bwawa moja linampatia Sh 25 milioni baada ya miezi michache.
Ametoa mwito kwa vijna kufanya ujasiriamali kwa guvu zote bila kusubiri ajira ambazo kwa kawaida siyo nyingi katika nchi zote duniani.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe Albert Chalamila , amesema wakuu wa mikoa waliamua kumwalika yeye kufunga maonyesho hayo baada ya kuvutiwa na uadilifu wake na kwamba Pinda ni kiongozi mwadilifu wa kuigwa na viongozi wasasa.
Mhe. Chalamila amekemea viongozi wanaoendekeza rushwa na uzembe katika Serikali ya awamu ya Tano na kwamba hawana budi kuacha mara moja badala yake watekeleze maagizo na maelekezo ya Rais John Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa