Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Hamis Kigwangala, amemshauri Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, kukaa na wakuu wa wilaya za Chunya na Songwe ili kumaliza tofauti zao zinazokwamisha usimamizi wa misitu iliyopo kwenye mipaka ya wilaya hizo.
Wakuu wa Wilaya hizo, Rehema Madusa wa Chunya na Samwel Opulukwa wa Songwe, wamekuwa hawaelewani kwa kipindi kirefu kutokana na mkanganyiko wa mipaka na usimamizi wa Msitu wa Hifadhi wa Patamela.
Madusa amekuwa akimlalamikia Opulukwa kuwa anawakamata waharifu wa msitu huo wa hifadhi wanaotoka Chunya na kuwapeleka wilayani kwake Songwe kwa ajili ya kuwachukulia hatua za kisheria akidai kuwa kitendo hicho ni kumwingilia katika Wilaya yake.
Akizungumza wakati wa Ziara yake ya kikazi wilayani Chunya, Dk. Kigwangala, alisema mgogoro huo ulishafikishwa ofsini kwake kwa ajili ya kuushughulikia lakini akamtaka Makalla kuwakutanisha viongozi hao kwa ajili ya kuweka uhusiano mwema.
“Suala la mgogoro wa viongozi hawa lilifika mpaka bungeni, lakini kubwa ni kwamba Madusa analalamika kuwa anaingiliwa kwenye mipaka yake, naomba muelewe kuwa msitu huu unasimamiwa na sheria moja na tangazo moja hivyo ni jukumu la kamati za ulinzi na usalama za wilaya zote kuusimamia,” alisema Dk. Kigwangala.
Hata hivyo alimtaka Madusa kusimamia sheria ili kulinda raslimali za taifa kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo badala ya kuingia kwenye migogoro isiyokuwa ya lazima.
Vilevile Dk. Kigwangala, alishangazwa na wananchi wa vijiji vilivyo jirani na msitu huo wa Patamela kutaka wakikamatwa washughulikiwe na Mkuu wa Wilaya ya Chunya badala ya Mkuu wa Wilaya ya Songwe ambapo alisema kitendo hicho kinaonyesha kuwa kuna udhaifu upande wa Chunya.
Alisema ni mara ya kwanza kuwasikia wananchi wakichagua mahali pa kushughulikiwa na kwamba kitendo hicho kinaonyesha uimara wa Mkuu wa Wilaya ya Songwe kwenye usimamizi wa sheria na udhaifu kwa Mkuu wa Wilaya ya Chunya.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, alisema amekubali ushauri wa waziri na ataanza kushuguhulikia mgogoro huo haraka ili kuimarisha ujirani mwema na utendaji kazi wa viongozi hao.
Alisema mgogoro huo anaufahamu vizuri kwa madai kuwa uliibuka kipindi ambacho alikuwa anaongoza mikoa yote miwili akiwa kama Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Songwe.
Alisema aliwaita viongozi hao wote na kuwasuluhisha lakini bado mgogoro huo ukafika mpaka bungeni lakinia akaahidi kuutumia ushauri wa Dk. Kigwangala kwa ajili ya kuumaliza.
“Tulishaanza kuushughulikia mgogoro huu, lakini ushauri wako utatuongezea nguvu na haraka sana tutaitana na kuwasuluhisha ili tuendelee na kazi zingine za maendeleo,” alisema Makalla.
Awali kabla Dk. Kigwangala hajatoa ushauri huo, wananchi waliohudhuria kwenye Mkutano huo, walibeba mabango mbalimbali yaliyokuwa yanamlalamikia Mkuu wa Wilaya ya Songwe kuwakamata huku wengine wakidai kuwa kitendo hicho kinaikosesha wilaya hiyo mapato.
Mmoja wa wananchi hao, Jastin Lucas, wamekuwa wakikamatwa na maaskari wa upande wa Wilaya ya Songwe na kupelekwa kupelekwa kwenye kituo cha Polisi cha wilaya hiyo badala ya Chunya hivyo akadai kuwa kitendo hicho ni unyanyasaji.
2 Barabara ya Kamishina, 53180 MBEYA
Anuani ya Posta: P. O.Box 754,Mbeya.
Simu: 025-2504045
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras@mbeya.go.tz
Haki Miliki©2023 Mkoa wa Mbeya. Haki zote Zimehifadhiwa